1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaishindilia Italia 5 - 1

11 Julai 2022

Ufaransa ililibamiza Italia mabao matano kwa moja na kuikamilisha duru ya Kwanza ya mechi za makundi ya mashindano ya Kombe la Ulaya kwa Wanawake. Duru ya kwanza ya mechi za makundi imekamilika.

https://p.dw.com/p/4DySG
Frauen-Fußball-EM: Deutschland - Dänemark
Picha: Heiko Becker/HMB Media/picture alliance

Kocha wa Italia Milena Bertolini amesema hakutarajia kushushiwa kipigo cha aina hiyo. "Bila shaka sikudhania kuwa ningekutana na Ufaransa na kupoteza 5 -0 baada ya kipindi cha kwanza. Hakika sikudhania hilo. Tulijua kuwa mechi hiyo ingekuwa ngumu sana kwa sababu Ufaransa ni timu imara kabisa, yenye wachezaji wazuri mno na wenye uwezo mkubwa wa kibinafsi."

Ushindi huo unaiweka Ufaransa usukani mwa Kundi D baada ya Ubelgiji na Iceland kutoka sare ya 1-1 katika mechi yao ya ufunguzi.

Duru ya pili ya mechi za makundi inaanza leo huku wenyeji England wakicheza dhidi ya Norway baada ya wote wawili kushinda mechi zao za ufunguzi. Austria inacheza dhidi ya Ireland Kaskazini katika mechi nyingine ya Kundi A.

Wafcon

Tuangalie sasa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake yanayoendelea nchini Morocco. Nigeria imetinga robo fainali baada ya kuichakaza Burundi 4 – 0 jana usiku.

Ushindi huo mnono umewapa matumaini makubwa baada ya kichapo cha siku ya ufunguzi dhidi ya Afrika Kusini. Nigeria itacheza dhidi ya Cameroon Alhamisi kutafuta tiketi ya nusu fainali na hivyo kufuzu moja kwa moja katika Kombe la Dunia la mwaka ujao nchini Australia na New Zealand. Burundi ambao walishiriki kwa mara yao ya kwanza, wametoka baada ya kupoteza mechi zote tatu. Afrika Kusini ilitinga robo fainali baada ya kuifunga Botswana 1 – 0.

Sasa watakabana koo na Tunisia ambao walifuzu pamoja na Botswana kama timu mbili bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi yao. Botswana ina kibarua kikali dhidi ya Morocco iliyoshinda mechi zote tatu za Kundi A. washindi wa Kundi B Zambia watacheza dhidi ya Senegal kutafuta tiketi ya nusu fainali.

dpa, reuters