1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaadhimisha miaka 158 tangu kupiga marufuku utumwa.

Mohamed AbdulRahman10 Mei 2006

Zaidi ya miaka 158 baada ya Ufaransa kupiga marufuku utumwa, baadhi ya waafrika wanajiuliza jee kuna mabadiliko makubwa yaliofanyika. Ufaransa leo ikiungana na baadhi ya makoloni yake pamoja na maeneo ya n´gambo yalio chini ya himaya yake,inaadhimisha siku iliopiga marufuku utumwa.

https://p.dw.com/p/CHnM
Picha ya zamani ya soko la watumwa
Picha ya zamani ya soko la watumwaPicha: AP

Siku hiyo inaandamana na tarehe iliochaguliwa na Rais Jacques Chirac kuadhimisha kupitishwa sheria mwaka 2001, inayotambua kwamba biashara ya utumwa ni uhalifu dhidi ya binaadamu..

Wakati siku hiyo ya kupigwa marufuku utumwa miaka 158 iliopita ikiadhimishwa leo, vijana wa kiafrika wanaokabiliwa na kifo kila mwaka wakati wakijaribu kuvuka mwambao wa bara la Afrika kwa mashua kuingia ulaya wanahisi kwamba makosa yaliofanywa na wakoloni yamefungua njia ya aina mpya wa utumwa mambo leo.

Mmoja wa wasimamizi wa jumba la makumbusho ya utumwa katika kisiwa cha Goree nchini Senegal Eloi Coly, mahala ambako iadadi kubwa isiojulikana ya watumwa walisafirishwa ,wengi wakielekea Marekani na katika makoloni ya Ufaransa katika eneo la Caribbean baina ya karne ya 16 na ya 19, anasema kuna hisia kwamba Ufaransa inahitaji au inanufaika na umasikini na ujinga ulioko Afrika.

Anaongeza kwamba pale ufaransa ilipotaka kujiendeleza baada ya vita vya pili ya dunia iliwakaribisha wafanyakazi na vibarua kutoka Afrika. Lakini sasa wanafikiria kwamba wahamiaji ndiyo chanzo cha ukosefu wa kazi na matatizo ya makaazi nchini mwao.

Baada ya Ureno, Uhispania na Uingereza, Ufaransa ni nchi ya nne ilionufaika kutokana na ishara ya utumwa barani Ulaya.

Pamoja na hayo Alioune Time katibu mkuu wa Jumuiya ya haki za waafrika-RADDHO anasema ni jambo la kufurahisha kwamba Ufaransa imetambua kuwa utumwa ni uhalifu dhidi

ya binaadamu, lakini bado kuna ukosefu mkubwa wa maarifa na elimu juu ya historia ya yaliofanyika.

Ufaranasa ilipiga marufuku utumwa 1794, lakini Napoleon Bonaparte akairudisha tena biashara hiyo 1802, labla ya kupigwa marufuku kabisa 1848.

Mhamiaji mmoja wa kiafrika nchini Ufaranasa alikua na haya ya kueleza juu ya umuhimu wa kuvifunza vizazi viliopo na vijavyo juu ya yaliotokea, akisema,"Ndiyo ninataka kuwaeleza watoto wangu nini utumwa. Leo hii mimi ni raia wa Ufaransa, lakini mababu zangu wanatoka Afrika na wakapelekwa katika visiwa vya Ufaransa huko Caribbean Walikua na uhaba wa chakula . Wafaransa kwa kweli hawakua watu wema.“

Rais Jacques Chirac leo alitarajiwa kuungana na Wafaransa wengine mjini Paris kuwakumbuka wahanga wa utumwa. Mkoloni mwengine wa zamani Uingereza, kwa upande awake itaadhimisha miaka 200 tangu kuupiga marufuku utumwa,mwaka ujao.