1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kuchunguza kifo cha Arafat

29 Agosti 2012

Waendesha mashitaka nchini Ufaransa wamefungua uchunguzi wa tuhuma za mauwaji ya aliyekuwa Rais wa Palestina Yasser Arafat mwaka 2004.

https://p.dw.com/p/15z5L
Jassir Arafat 2004Picha: picture-alliance/dpa

Uchunguzi huo unafuatia madai ya mauwaji kutoka kwa mjane wa kiongozi huyo, Bibi Suha Arafat. Nayo mamlaka ya utawala wa Palestina imeukaribisha uchunguzi huo.

Kufunguliwa kwa uchunguzi huo kunafutaia madai yaliyotolewa na mjane wa kiongozi huyo Suha Arafat kuwa huenda kifo cha mume wake kilitokana na sumu. Familia ya Arafat ilifungua madai ya kisheria nchini Ufaransa mwezi uliopita.

Suha Arafat, mkane wa marehemu Yasser Arafat
Suha Arafat, mkane wa marehemu Yasser ArafatPicha: AP

Uchunguzi uliofanywa mwaka jana unaonyesha kuwa huenda Arafat alikufa kutokana na mionzi aina ya Polonium. Madini ya Polonium ni sumu kali, na ndio yaliyotumika kumuuwa mpelelezi wa zamani wa Urusi Alexander Litvinenko mjini London, Uingereza mnamo mwaka 2006.

Uthibitisho wa mwendesha mashitaka

Mwendesha mashitaka msaidizi Caroline Chassain amelithibitishia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kuwa ofisi yake katka eneo la Nanterre magharibi mwa mji wa Paris imeamuru uchunguzi huo ufanyike.

Uchunguzi huo utaendeshwa na hakimu mmoja au zaidi wenye uzoefu wa kazi hiyo ambao pia ndio watakaokuwa na mamlaka ya kukusanya ushahidi.

Madai ya mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel kupewa sumu yalifufuka mwezi uliopita baada ya kituo cha televisheni cha Aljazeera kuonyesha uchunguzi ambao wataalamu walisema kuwa wamekuta kiasi kikubwa cha madini ya Polonium kwenye nguo, kilemba na vitu vingine vya marehemu.

Marehemu Yasser Arafat
Marehemu Yasser ArafatPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza na kituo hicho mwanasheria wa familia ya Arafat Pierre Olivier Sur amesema: "Naamini kuwa serikali ya Ufaransa inatakiwa kulibeba suala hili, na mahakama nchini Ufaransa ifukue na kuchunguza mabaki ya mwili wa Arafat, ili kujua kiwango cha sumu ambayo inasemekana alipewa bwana Arafat."

Maabara ya kisayansi ya radiolojia katika Chuo Kikuu cha hospitali ya Lausanne nchini Uswis ambayo imeshiriki katika uchunguzi huo, imesema kuwa imepokea ruhusa kutoka kwa Bibi Suha ya kuendelea na uchunguzi zaidi wa mabaki ya Arafat kujua kuhusu sumu hiyo ya Polonium. Mjane huyo ameruhusu pia kufukuliwa kwa mabaki ya mwili wa marehemu mumewe katika kaburi alikozikwa kwenye mji wa Ramallah, Ukingo wa Magharibi.

Waziri wa sheria wa Palestina Ali Muhanna ameiambia DPA kuwa ingawa maamuzi hayo yamechelewa kuchukuliwa, lakini hiyo ndiyo hatua sahihi katika mwelekeo sahihi. Anasema kuwa hospitali hiyo ya Ufaransa ndiyo inajuwa zaidi ukweli na chanzo cha kifo cha Arafat.

Hakuna ushaidi: Madaktari wa Ufaransa

Jana mtandao wa habari wa Ufaransa, Slate.fr, ulichapisha nakala ya ripoti ya kitabibu kuhusu kifo cha Arafat na kusema kuwa dalilizake hazionyeshi uhusiano wowote na sumu ya Polonium. Mkuu wa zamani kitengo cha Rheumatologia katika hospitali hiyo Marcel Francis -Kahn ameuambia mtandao huo kuwa Arafat hakuwa na dalili za kawaida za mtu aliyepewa mionzi za kunyonyoka nywele.

Jiji la Paris nchini Ufaransa.
Jiji la Paris nchini Ufaransa.Picha: picture alliance/abaca

Marehemu Arafat alipelekwa katika hospitali ya kijeshi ya Percy nje kidogo ya jiji la Paris baada ya kusumbuliwa na kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo, kuharisha na kiwango cha chini cha chembe za damu ambacho si cha kawaida.

Madakatari kwenye hospitali hiyo walimfanyia vipimo kadhaa lakini hawakuweza kugundua kwa uhakika sababu ya maradhi yake. Siku chache baada ya kufika hospitalini , Arafat alipoteza fahamu na baadaye kufariki tarehe 11 Novemba 2004.

Mwandishi: Stumai Goerge/DPA/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed