1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yakabiliwa na mbinyo kuhusu ubaguzi wa rangi

25 Oktoba 2013

Chama cha kutetea maslahi ya wachezaji wa soka ya kulipwa ulimwenguni – FIFPro kimelishtumu Shirikisho la Soka barani Ulaya UEFA kwa kushindwa kutekeleza mwongozo kuhusiana na tabia ya ubaguzi wa rangi

https://p.dw.com/p/1A6Hy
Rais wa UEFA Michel Platini anasema watachukua hatua kali dhidi ya matukio ya kibaguzi
Rais wa UEFA Michel Platini anasema watachukua hatua kali dhidi ya matukio ya kibaguziPicha: AFP/Getty Images

Hii ni kutokana na kisa ambacho mchezaji wa Manchester City Yaya Toure anadaiwa kuwa mwathiriwa ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa klabu ya CSKA Moscow katika mchuano wa katikati ya wiki wa Champions League.

FIFPro imesema waamuzi wa UEFA katika mchuwano huo walishindwa kuchukua hatua baada ya Toure kulengwa na mashabiki wa CSKA Moscow waliomtolea matamshi ya kibaguzi. UEFA ilitoa mwongozo Julai 2009 ikiwapa waamuzi wa mechi mamlaka ya kusitisha na kumaliza michuwano kama kuna tukio kuu la kibaguzi. Hatua tatu zinazostahili kufuatwa ni kwanza, refarii asimamishe mechi na kuomba tangazo lifanywe uwanjani kupitia spika za uwanja kuwaambia mashabiki kuwacha tabia hiyo.

Hatua ya pili ni kusitisha mechi kwa muda Fulani na kisha kuumaliza mpira kabisa. Mwezi Machi mwaka huu, UEFA ilitoa azimio lililowataka waamuzi kuzingatia mwongozo huo. Lakini hakuna mchuano wowote uliowahi kusitishwa katika dimba la Ulaya tangu mwongozo huo ulipozinduliwa.

Toure alisema mashabiki waliiga milio ya nyani. UEFA ilisema hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya CSKA Moscow baada ya uchunguzi kukamilika. Klabu ya CSKA imesema baada ya kuchunguza video zote za uwanjani hawajapata ushahidi wowote wa kuwepo matamshi au matendo ya kibaguzi kutoka kwa mashabiki wake.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP/reuters

Mhariri: Yusuf Saumu