Uchaguzi wa bunge la Ulaya vyama vya kihafidhina vyachelekea.
8 Juni 2009Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema leo kuwa mafanikio ya chama chake katika uchaguzi wa bunge la Ulaya umeimarisha nafasi yake ya kushinda kipindi cha pili cha madarakani wakati Ujerumani itakapofanya uchaguzi mkuu wa taifa Septemba mwaka huu.
Merkel ameonekana kuwa na furaha kubwa alipowaambia waandishi habari kuwa matokeo haya yanatupa ujasiri , nguvu na kujiamini ili kuweza kusonga mbele na nafasi yetu katika uchaguzi mkuu imeongezeka bila shaka tangu uchaguzi wa jana.
Matokeo ya mwisho yaliyotolewa siku ya Jumatatu yanaonyesha kuwa chama cha kansela Angela Merkel cha Christian Democratic CDU, na chama ndugu cha jimbo la bavaria cha CSU kwa pamoja vimepata asilimia 37.9 ya kura wakati hasimu wao mkubwa chama cha Social Democratic SPD kimeanguka hadi asilimia 20.8.
Pengo lililopo kati ya CDU na SPD, limekuwa kubwa mno na kufikia asilimia 17, Merkel amesema.
Napenda kusema wazi kuwa uchaguzi huu si jaribio la uchaguzi mkuu, lakini unaonyesha mwelekeo, na tungependa kutumia mwelekeo huu kufanyia kazi katika wiki zijazo hadi wakati wa uchaguzi mkuu. Na matokeo ya uchaguzi huu yanatupa ujasiri nguvu na kujiamini.
Wakati huo huo viongozi wa chama cha SPD wamejaribu kujifariji kutokana na kuanguka katika uchaguzi wa bunge la Ulaya , ambao umeelezwa katika vyombo vya habari kuwa ni maafa makubwa.
Ni jioni mbaya sana kwetu kwa kuwa matokeo ni mabaya kuliko tulivyotarajia na inasikitisha, bila shaka.
Akikiri kuwa matokeo hayo yanakatisha tamaa, kiongozi wa chama cha SPD Franz Muenterfering amewaambia waandishi habari, kuwa kile kilicho wazi ni kuwa tunaendelea kushikilia kwa nguvu msimamo wetu wa kisiasa.
Wakati huo huo waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown anakabiliwa na changamoto kali katika uongozi wake leo baada ya uungwaji mkono wa chama chake kuporomoka katika kiwango chake cha chini kabisa katika muda wa karne katika uchaguzi wa Ulaya.
kuporomoka kwa kura za chama cha Labour, ambako kumefuatia kufanya vibaya katika uchaguzi wa serikali za mitaa wiki iliyopita, kumesaidia chama chenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia cha British National Party BNP kushinda viti viwili katika bunge la Ulaya, ikiwa ni mara ya kwanza kuweza kuwakilishwa katika bunge hilo.
Brown atakabiliana na wabunge wa chama cha Labour leo jioni , baadhi yao wakiwa wanaukosoa wazi utaratibu wake wa uongozi na kumtaka ajiuzulu ili kutoa nafasi kwa chama hicho kupambana katika uchaguzi mkuu ujao, ambao unatarajiwa kufanyika Juni 2010.
Mawaziri sita waandamizi wamejiuzulu wiki iliyopita na naibu waziri mmoja Jane Kennedy alikuwa ni waziri wa mwisho kujiuzulu leo Jumatatu akisema kuwa amechoshwa na vitisho, uonevu na ukandamizaji, vitu ambavyo anasema vinaendeshwa na ofisi ya Brown.
Nae waziri mkuu wa Hispania amesema kuwa serikali yake ya chama cha Kisoshalisti imetambua kuporomoka kwake baada ya kushindwa katika uchaguzi huo kwa chama cha upinzani cha kihafidhina.
►◄