1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Libya kufanyika mwaka ujao

14 Novemba 2018

Waziri wa mambo ya kigeni wa Italia, Enzo Moavero amesema Libya huenda ikafanya uchaguzi katika kipindi cha machipuko mwaka ujao. Ameyasema hayo katika mkutano wa siku mbili mjini Palermo wa kujaribu kuleta amani Libya.

https://p.dw.com/p/38DZH
Fayez al-Serraj
Fayez Siraj kiongozi wa serikali Mjini Tripoli na Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe ContePicha: Imago/C. Minelli

Makundi yanayohasimiana Libya, yalikutana kwa mara ya kwanza kwa muda wa zaidi ya miezi mitano mjini Sicily hapo jana huku Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte akiwasilisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa kufanyika uchaguzi mwaka 2019.

Hata hivyo haijawa wazi iwapo kukutana kwao kutaleta mabadiliko ya kweli katika mgogoro  wa kisiasa unaoikumba Libya.

Ghassan Salame
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Libya Ghassan Salame Picha: picture-alliance/AP Photo/Thein Zaw

Kulingana na mjumbe ambaye hakutaka jina lake litajwe, mazungumzo hayo  yalisababisha Jenerali Khalifa Hiftar ambaye ni kamanda wa jeshi aliloliunda mwenyewe la LNA  linalolidhibiti  eneo la Mashariki mwa Libya, kukubali Fayez Siraj anaeongoza serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilioko Mjini Tripoli, anaweza kuendelea kushikilia nafasi yake hadi pale uchaguzi utakapofanyika.

Pande mbili zinazohasimiana Libya, zinahimizwa kusitisha mapigano

Waziri Mkuu wa Italia Giuseppe Conte amesema bado ni muhimu uchaguzi ufanyike kwa kuweka mbele usalama na kuheshimu mahakama na katiba. Kwa upande wake Ghassan Salame mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Libya ameonya ama mchakato wa kisiasa usonge mbele au mapigano mapya huenda yakatokea wakati wowote.

Taarifa ya pamoja ilitaja umuhimu wa kufanyika uchaguzi kati ya mwezi Machi na Juni mwaka ujao na kuzihimiza pande zote zinasohasimiana zisitishe vurugu.

Libyen Khalifa Haftar LNA Kommandeur
Kamanda wa jeshi la LNA Jenerali Khalifa HaftarPicha: picture-alliance/TASS/S. Savostyanov/TASS

Mazungumzo hayo ya pande hizo mbili zinazohasimiana nchini Libya yalihudhuriwa pia na rais wa Tunisia Bejd Caid Essebsi, Waziri Mkuu wa Urusi na Algeria Dmitry Medvedev na Ahmed Ouyahia, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian na Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk.

Mjumbe maalum wa Mataifa kwaajili ya Libya Ghassan Salame na rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi pia walihudhuria.

Claudia Gazzini, mchambuzi wa masuala ya Libya katika shirika la kimataifa la kushughulikia migogoro amesema iwapo kutakuwa na makubaliano ya kweli kati ya Haftar na Fayez Siraj basi hatua kubwa itakuwa imepigwa katika juhudi za kuleta amani nchini Libya.

Mwandishi:  Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman