1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uamuzi wa Mahakama ya juu wawapa hofu viongozi wa dini Kenya

27 Februari 2023

Viongozi wa Makanisa ya Kiinjili, Kenya wamekosoa uamuzi wa Mahakama ya juu kuwaruhusu watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kuwa na mashirika yao wakiutaja uamuzi huo kama unaolenga kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja

https://p.dw.com/p/4O18t
Kenia wartet mit Spannung auf das Urteil des Obersten Gerichtshofs zu den Wahlen
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP

Mdahalo wa mapenzi ya watu wenye jinsia moja unazidi kuwa kiazi moto katika taifa ambalo asilimia 80 ya raia wake ni wakristo, siku chache tu baada ya Mahakama ya Juu kuamua kuwa watu hao wana uhuru wa kuunda mashirika na kutangamana kwa uhuru. Sasa makundi ya dini yamejitokeza kupaza sauti zao dhidi ya uamuzi huo.

Daktari David Oginde mwenyekiti wa makanisa ya  Kiavanjeli nchini Kenya alisema kwamba wanalaani uamuzi wa Mahakama ya Juu na idadi kubwa ya majaji walioshikilia uamuzi huo, kwani uamuzi huo unafungua mwanya wa kuhalalisha vitendo vya watu wa jinsia moja ikiwemo ndoa zao.

Mahakama Kenya yapinga kupima mashoga

Viongozi hao sasa wanasema wanatafuta ushauri kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kubatilisha uamuzi huo ambao wanasema ni kinyume cha katiba ya nchi, huku wakitoa wito kwa viongozi wote kuungana kulaani uamuzi huo. Viongozi hao pia wanasema watawasilisha ombi katika bunge la Taifa, kuunda sheria zinazozuia vitendo vya watu wa jinsia moja. Sasa wanataka wafanye kikao na majaji watatu waliohusika kupitisha uamuzi huo kupata maelezo zaidi.

Wahusika wautaja uamuzi huo kama ushindi

Kenia | LGBTQ | ugandische Flüchtlinge in Kakuma
Bendera inayowatambulisha watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia mojaPicha: Sally Hayden/ZUMA/imago images

Kwenye uamuzi wao uliotolewa Ijumaa, majaji watatu kati ya watano waliamua kuwa watu wa jinsia moja wana haki ya kutangamana licha ya kuwa ni kinyume cha sheria kwa ndoa zao na pamoja na tendo la unyumba nchini Kenya. Wawakilishi wa makundi hayo wametaja uamuzi huo kama ushindi. Kanyali Mwikya na Essy ni wanaharakati wa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja.

NAIROBI:Viongozi wa kanisa Anglikana barani Afrika watofautiana juu ya mwito wa wenzao wa Marekani kuhusu Ushoga

Ikitoa uamuzi huo Mahakama ya Juu ya Kenya ilisema kuwa uhuru wa kutangamana ni haki ya binadamu katika jamii yoyote inayozingitia demokrasia.

Hata kabla ya ombi la viongozi wa kievanjeli kufikishwa kwenye bunge, Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma amemwandikia barua spika wa bunge Moses Wetangula akitaka wahusika wa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja kuadhibiwa vikali. Amependekeza watakaopatikana kufungwe maisha.

Mwandishi: Shisia Wassilwa