1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za Afrika zitakazoshuka dimbani Brazil

1 Juni 2014

Timu tano zilizofuzu kuliwakilisha bara la Afrika katika dimba la Kombe la Dunia nchini Brazil - Cote d'Ivoire, Cameroon, Ghana, Nigeria na Algeria, zina matumaini ya kuwashangaza wengi katika tamasha hilo

https://p.dw.com/p/1C2uW
Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Elfenbeinküste
Picha: picture alliance/abaca

Cote d'Ivoire

Didier Drogba anafahamu kuwa siku zake za kucheza katika Kombe la Dunia zinadidimia na kwamba dimba la Brazil 2014 huenda likawa fursa yake ya mwisho kuichezea Cote d’Ivoire.

Drogba na wenzake mara nyingi hawajakuwa na bahati wakati wa kupangwa makundi katika vinyang’anyiro viwili walivyoshiriki. Katika mwaka wa 2006, walipangwa na Argentina, Uholanzi na Serbia na Montenegro katika duru ya kwanza. Na nchini Afrika Kusini, wapinzani wao katika awamu ya makundi walikuwa Brazil, Ureno na Korea Kaskazini.

Timu hiyo ya Mfaransa Sabri Lamouchi inataraji kuwa mara hii safari yao itamwendea vyema nahodha wao Didier Drogba mwenye umri wa miaka 33. Timu hiyo inajivunia majina ya kimataifa kama vile Yaya Toure, Salomon Kalou, Gervinho na wengine wengi. Licha ya ubora huo wa hali ya juu, hata safari yao ya kuelekea Brazil ilikuwa ngumu kuliko ilivyotarajiwa. Baada ya matatizo kidogo katika awamu ya makundi, Cote d’Ivoire karibu wabanduliwe nje kupitia mechi ya mchujo dhidi ya Senegal lakini Kalou akafunga katika dakika ya mwisho na kuwapa tikiti ya kuelekea Brazil.

Na mara hii The Elephants wamepangwa katika kundi C pamoja na Ugiriki, Japan na Colombia.

Ghana

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Ghana
Ghana iliondolewa katika robo fainali mwaka wa 2010Picha: picture alliance/AP

Ghana wametambulika kama mojawapo ya timu bora zaidi za soka barani Afrika kwa miaka kadhaa sasa, baada ya kudhihirisha mchezo wa hali ya juu katika Kombe la Dunia mwaka wa wa 2006 na 2010.

The Black Stars wanataraji angalau kufuzu katika awamu ya mwondowano kwa mara ya tatu mfululizo katika dimba la mwaka huu. Ghana iliibaza Jamhuri ya Czech na Marekani katika Kombe la Dunia mwaka wa 2006 nchini Ujerumani, kanla ya kuzidiwa nguvu na mabingwa mara nyingi Brazil katika raundi ya 16 bora. Nchini Afrika Kusini, Black Stars walikuwa timu pekee ya Afrika kufuzu kutoka awamu ya makundi. Waliizaba Marekani tena kabla ya kuzidiwa nguvu na Uruguay kupitia mikwaju ya penalty katika robo fainali. Licha ya kufanya vibaya katika Kombe la Mataifa ya Afrika, maafisa wa soka nchini humo waliamua kusalia na kocha James Kwesi Appiah.

Barabara ya kufika Brazil ilikuwa na changamoto lakini Ghana iliweza kuwapiku Misri katika mechi ya mchujo. Vijana hao kama wangepenga kufanya vyema nchini Brazil, watahitaji mchezo mzuri kutoka kwa wachetaji wake kama vile Michael Essien wa AC Milan, Kwadwo Asamoah wa Juventus, Kevin-Prince Boateng wa Schalke na Asamoah Gyan.

Wapinzani wa Ghana katika Kundi G ni Ujerumani, Ureno na Marekani.

Cameroon

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Kamerun
Cameroon inalenga kudhihirisha usogora wake katika jukwaa la kimataifaPicha: picture alliance/AP

Cameroon walipambana vita vikali vya kufuzu lakini mwishoni wakajipa nafasi ya kushiriki kwa mara ya saba katika Kombe la Dunia. Na Indomitable Lions wako Brazil wakiwa na matarajio yenye majivuno.

"Kama tutafanya kazi ipasavyo, ili tunaweza kuanya vyema zaidi kuliko kilichofanywa na Ghana miaka mitatu iliyopita nchini Afrika Kusini". Hayo ni maneno gwiji Samuel Eto’o. Hiyo itamaanisha kuwa waweze kufuzu katika nusu fainali ya Kombe la Dunia baada ya Ghana kufika robo fainali mwaka wa 2010. Eto’o aliisaidia Indomitable Lions kupata ushindi wa jumla ya magoli manne kwa moja dhidi ya Tunisia katika mechi za mchujo.

Kando na kufika katika robo fainali kwa usaidizi wa Roger Milla mwaka wa 1990, Cameroon wamepata ushindi mmoja pekee katika vinyang’anyiro vingine vitano na hawajawahi kuondoka katika awamu ya makundi. Haikuwa imefikiriwa kuwa Eto’o angeichezea tena Cameroon baada ya kutangaza kustaafu kutoka soka la kimataifa. Shirikisho la soka la Cameroon pia lilisitishwa na FIFA kwa madai ya serikali kuingilia masuala ya timu. Lakini adhabu hiyo iliondolewa wiki tatu baadaye. Kando na Eto’o kocha Mjerumani Volker Finke ana vipaji muhimu kikosini ikiwa ni pamoja na Eric Maxim Choupo-Moting, Pierre Webo, Nicolas N'Koulou, Alexandre Song na Jean Makoun.

Cameroon lazima wakuane na wenyeji Brazil, Croatia na Mexico katika kundi A.

Nigeria

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Nigeria
Mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika wana matumaini ya kufanya vyema nchini BrazilPicha: picture alliance/augenklick

Nigeria haikuwa na maandalizi mazuri ya Kombe la Dunia nchini Brazil 2014 na hata meneja Stephen Keshi ni mmoja wa wasiojuwa kinachoweza kutarajiwa kutoka kwa Super Eagles.

Mgogoro kuhusu marupurupu uliyagubika maandalizi ya Kombe la Mashirikisho mwaka wa 2013 na kisha Super Eagles wakabanduliwa nje ya duru ya kwanza ya dimba hilo.

Mabingwa hao wa Afrika Nigeria walirejea tena na kuwapiku Ethiopia katika mechi za mchujo ili kujikatia tikiti ya kwenda Brazil. Huku wakishiriki Kombe la Dunia kwa mara yao ya tano, nahodha wa Nigeria kwa mara nyingine atakuwa kungo nyota wa Chelsea John Obi Mikel. Nchi hiyo ina matarajio mengi kumhusu mchezaji Sunday Mba, anayecheza ligi ya nyumbani.

Watalaamu wengi wanaiona Nigeria kuwa timu yenye vipaji vingi barani Afrika na ambayo inaweza kuwaduwaza miamba wa Amerika ya Kusini na Ulaya. Lakini Super Eagles pia wanafahamika kwa ukosefu wa nidhamu uwanjani. Nigeria wamepangwa katika kundi F pamoja na Argentina, Iran na Bosnia- Herzegovina.

Algeria

Interaktiver WM-Check 2014 Mannschaft Algerien
Timu pekee iliyofuzu kutoka Kaskazini mwa AfrikaPicha: picture alliance/dpa

Algeria wamekumbwa na mchanganyiko wa mafanikio na changamoto katika vinyang’anyiro vyao viwili vya awali vya Kombe la Dunia, lakini kizazi kipya kinachoongozwa na nahodha Madjid Bougherra kinatumai kuweka mafanikio mapya nchini Brazil.

Algeria waliwapata sifa kwa kuwachabanga mabingwa wa wakati huo wa Ulaya Ujerumani ya Magharibi katika mchuano wao wa kwanza kabisa wa Kombe la Dunia mwaka wa 1982. Katika mechi ya mwisho ya makundi, Wajerumani waliwapiku Austria goli moja kwa sifuri katika mechi yenye utata iliyozipa timu hizo mbili za Ulaya kibali cha kufuzu katika duru iliyofuata nao Algeria wakarejea nyumbani.

Katika mwaka wa 1986, Algeria ilifunga goli moja tu na kupata pointi moja kabla ya kurejea nyumbani. Nchini Afrika Kusini, Algeria waliwateka Uingereza kwa sare ya kutofungana goli na kisha karibu wawabanduwe Marekani hadi pale goli la dakika ya mwisho katika kipindi cha pili lake Landon Donovan lilipowapa Wamarekani ushindi wa goli moja kwa sifuri, na wakatolewa tena mapema.

Kocha Vahid Halilhodzic atamtegemea Bougherra kuwaongoza wenzake uwanjani kutokana na sifa zake beki huyo asiyeleta mzaha uwanjani. Algeria wana kibarua dhidi ya Ubelgiji, Urusi na Korea Kusini katika kundi H.

Mwandishi: Bruce Amani/dpa
Mhariri: Yusuf Saumu