1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu Ujerumani katika mtihani mkubwa dhidi ya Ufaransa

Sekione Kitojo
15 Oktoba 2018

Timu ya  taifa  ya  Ujerumani , Die Mannschaft imo  katika  mtihani mkubwa wakati ikijitayarisha  kupambana na mabingwa  wa  Dunia Ufaransa  kesho katika  ligi  ya mataifa ya Ulaya.

https://p.dw.com/p/36ajQ
UEFA Nations League - Niederlande gegen Deutschland | Nationaltrainer Löw
Picha: picture-alliance/GES/M. Ibo Güngör

Hali  ni  ya  kuporomoka  tu, ndivyo  wanavyosema  wakosoaji  wa kocha  wa  timu  ya  taifa  ya  Ujerumani Joachim Loew, wakitabiri kutokana  na  kuporomoka  kunakoendelea  tangu  pale kampeni  ya timu  ya  taifa  ya  Ujerumani  kugonga mwamba  na  kutolewa  na mapema  katika  michuano  iliyopita  ya  kombe  la  dunia. Kikosi chake  kimeshindwa  hadi  sasa  kupata  bao  katika  michezo  mitatu mfululizo ya  mashindano, kwa  mara  ya  kwanza  katika  historia  ya nchi  hii.

Fußball Länderspiel  Deutschland - Peru
Tony Kroos akimpongeza Julian Draxler (kulia)Picha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Ujerumani  imo  katika  hatari  ya  kushuka  daraja  kutoka  katika kundi  la  ligi  ya  mataifa  ya  Ulaya.

"Tunakosolewa  sana , na  mimi  kama  kocha  ninawajibika lakini kwa  namna  fulani  tunapaswa  kuziba  masikio  na  kuliondoa  hilo akilini  mwetu katika  siku  mbili kuelekea  katika  mchezo  mgumu dhidi  ya  mabingwa  wa  dunia  Ufaransa  kwa  kuwa  kwa  kweli ndio  nafasi  ya  mwisho,"  amesema  Joachim Loew.

Mabadiliko  yaliyoahidiwa  ya  aina  ya uchezaji  katika  timu hayajatokea. Licha  ya  matokeo  hayo  mabaya , baadhi  ya wachezaji  wakongwe  katika  timu  hiyo  wanaamini  kwamba  bado wanacheza vizuri.

Mats Hummels mlinzi  wa  kati  wa  Ujerumani  anasema, " naweza kushutumiwa  kuwa  sikosoi vya  kutosha  lakini  sifikiri  kwamba tumecheza  vibaya dhidi  ya  Uholanzi. Uholanzi  iliikandika Ujerumani  mabao 3-0 siku  ya  Jumamosi, na  kuiweka  Ujerumani katika  hali  ngumu  ikishika  mkia  katika  kundi  lao  ambalo  lina timu  za  Ufaransa  , Uholanzi  na  Ujerumani.

Fussball  England vs. Deutschland | Mats Hummels
Mats Hummels (kulia ) akitoa ushauri kwa Matthias Ginter (kushoto)kuhusu ulinziPicha: picture-alliance/SvenSimon/A. Wälischmüller

Tuna  wachezaji wenye  uwezo  mkubwa, kwa  kawaida  tuna  timu nzuri  ya  taifa, lakini  tunachukuliwa  kama  wachezaji  ambao si wa kulipwa.

Wachezaji wachanga

Lakini  baadhi  ya  wachezaji  wachanga  katika  timu  hiyo  ya  taifa wameeleza  kwa  njia  ya  kujikosoa  zaidi. Joshua Kimmich mlinzi  wa  Ujerumani  amesema , " Hatuwezi  kufanya  makosa  ya  kujisifu  kimchezo. Iwapo tunapoteza  michezo  katika hali  hii, haiwezi  kuwa  imetokea  ya  bahati  mbaya  tu."

Kuna  kitu  lazima  kibadilike , hilo  ni  wazi. iwapo  watacheza  vibaya  mara nyingine  dhidi  ya  Ufaransa kesho  Jumanne mashabiki  wengi  zaidi watataka  Loew  afungishwe  virago  na  kuiacha  timu.

Fußball WM 2014 Deutschland Frankreich Viertelfinale
Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier DeschampsPicha: Reuters

Sergio Ramos  nahodha  wa  timu  ya  taifa  ya  Uhispania amemsifu sana  mshambuliaji  wa  timu  ya  taifa  ya  England Harry Kane kuwa , kimwili  ni  mtu wa  ajabu, lakini  bado  anaipigia  upatu timu  yake ya  Uhispania  kwamba  itaendeleza ukame  wa  mabao  wa mshambuliaji  huyo  wa  England  leo  Jumatatu katika  mchezo  wa kundi  la 4.

Kikosi  cha  kocha  Luis Enrique kinaweza  kujihakikishia  nafasi  ya juu  ya  kundi  hilo kwa  ushindi, baada  ya  kuishinda  England  katika uwanja  wa  Wembley kwa  mabao  2-1  mwezi  uliopita . England inapambana  kuepuka  kushuka  daraja  kutoka  ligi A na inaweza kufanya  hivyo  ikiwa  Kane  ataweza  kuonesha  makali  yake.

Leo jioni  kuna  mapambano ya  ligi  ya  mataifa  ya  Ulaya  kati  ya Iceland ikiikaribisha  Uswisi , Finland inapambana  na  Ugiriki , Belarus  inaisubiri nyumbani  Moldovia, Bosnia Herzegovina ina miadi  na  Ireland  ya  kaskazini.

Fußball Champions League Finale 2018 / Real Madrid-FC Liverpool 3-1
Nahodha wa timu ya taifa ya Uhispania Sergio Ramos Picha: picture-alliance/SvenSimon/F. Hoermann

Poland  imekuwa  timu  ya  kwanza  kushuka  daraja  katika mashindano  yanayoendelea  ya  ligi  ya  mataifa  ya  Ulaya  baada ya  kupokea  kipigo  cha  bao 1-0  dhidi  ya  Italia  jana , Poland ikisalia  na  poiti  moja  tu  katika  kundi  la , wakati  Italia  ina  pointi 4   na  Ureno  ikishika  nafasi  ya  kwanza  ya  kundi  hilo  ikiwa  na pointi  6.

Urusi  ilipata  ushindi  wa  mabao 2-0  dhidi  ya  Uturuki mjini  Sochi na  kupata  udhibiti wa  kundi B katika  ligi  ya  pili, na  kufikisha mwisho  matumaini  ya Uturuki  kupata daraja la  A.

 

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape /afpe /dpae/

Mhariri: Iddi Ssessanga