1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May ahimiza mshikamano ndani ya chama chake

Grace Kabogo DPA, RTRE
3 Oktoba 2018

Theresa May amekitolea wito chama chake cha Conservative kumuunga mkono na kuiunganisha Uingereza. May amewataka wanachama hao kuunga mkono mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/35vdP
Birmingham Tory-Parteitag Rede Theresa May
Picha: Getty Images/AFP/P. Ellis

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amekitolea wito chama chake cha Conservative kumuunga mkono na kuiunganisha Uingereza ambayo imegawanyika kutokana na tofauti za maoni zilizochochewa na mpango wake wa Uingereza kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya. 

Akizungumza mjini Birmingham katika hotuba yake ya kuufunga mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha Conservative, May amewataka wanachama hao kuunga mkono mpango wake kuhusu mchakato wa Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit na kukijenga chama chenye heshima na cha kizalendo. Mpango huo wa Brexit unajulikana kama ''Chequers''.

Amekikosoa chama cha upinzani cha Labour na kumshutumu kiongozi wake, Jeremy Corbyn kwa kukataa mapendekezo ambayo yaliwahi mara moja kuwaunganisha wanasiasa waliokuwa wamegawanyika. May amesema wanahitaji kuwa chama kwa ajili ya nchi nzima, na sio chama cha wachache, lakini kwa kila mmoja ambaye yuko tayari kufanya kazi kwa bidii.

''Na kuna sababu nyingine kwa nini tunahitaji kuungana pamoja. Tunaingia katika awamu ngumu ya mazungumzo. Mliona Salzburg, kwamba niliisimamia Uingereza. Tunachopendekeza ni changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya, lakini kama tukiungana pamoja, najua tunaweza kupata makubaliano yenye tija kwa Uingereza.''

Je kuna mipango ya kumuondoa May madarakani?

Gazeti la Telegraph limeandika katika toleo lake kwamba baadhi ya wanachama wa ngazi ya juu wa Conservative wamejadiliana kuhusu mipango ya kumuondoa madarakani May kama atakataa kujiuzulu kabla ya mkutano mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2022.
Gazeti la Telegraph limeandika katika toleo lake kwamba baadhi ya wanachama wa ngazi ya juu wa Conservative wamejadiliana kuhusu mipango ya kumuondoa madarakani May kama atakataa kujiuzulu kabla ya mkutano mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2022.Picha: Getty Images/AFP/O. Scarff

Katika wiki za hivi karibuni, May amekumbana na changamoto katika uongozi wake, baada ya kukosolewa na waziri wa zamani wa mambo ya nje, Boris Johnson mwanaharakati anayepigania Uingereza kujiondoa kwenye umoja wa Ulaya pamoja na wanachama wengine wa Conservative wanaounga mkono msimamo mkali wa Brexit, wakitaka nchi hiyo ijitenge kabisa na Umoja wa Ulaya. Jana Johnson alimtaka May kuachana na mpango huo, na kushangiliwa sana na wajumbe wa mkutano huo.

Gazeti la Telegraph limeandika katika toleo lake la leo kwamba baadhi ya wanachama wa ngazi ya juu wa Conservative wamejadiliana mipango ya kumuondoa madarakani May kama atakataa kujiuzulu kabla ya mkutano mkuu uliopangwa kufanyika mwaka 2022.

Mwanaharakati wa kampeni ya Brexit na aliyekuwa kiongozi wa chama cha UK Independence, Nigel Farage ameandika katika mtandao wake wa Tweeter kuwa anatarajia May ataendelea kuiongoza nchi hiyo na kwamba Brexit itaendelea kuheshimiwa.

Baada ya hotuba hiyo ya May, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk amesema viongozi wa umoja huo watakutana kujadiliana kuhusu uwezekano wa mpango wa Brexit, katika chakula cha jioni kitakachofanyika mjini Brussels Oktoba 17. Tusk amesema May pia atahudhuria mkutano huo.

 

Mhariri: Iddi Ssessanga