1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yazindua mpango wa TASAF wa kunusuru kaya masikini

17 Februari 2020

Serikali ya Tanzania imezindua mpango wake wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu wa kunusuru kaya masikini nchini humo ujulikanao kama TASAF

https://p.dw.com/p/3Xu17
Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Picha: DW/E. Boniphace

Uzinduzi wa mpango huo ulioasisiwa takriban miongo miwili sasa, unakuja katika kipindi ambacho wadau mbalimbali wa maendeleo wakitaja kupanda kwa gharama za maisha katika taifa hilo la Afrika Mashariki, huku hali ya umasikini katika maeneo ya vijijini ikishamiri.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na umasikini, ambapo kina cha umasikini katika taifa hili la Afrika Mashariki ni asilimia 26.4.

Matokeo ya utafiti katika kitabu cha hali ya kiuchumi yanaonesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi ni mkubwa kwa maeneo ya vijijini kwa asilimia 31.3 ikilinganishwa na maeneo ya mijini yaliko asilimia15.8.

Rais John Magufuli, aliyezindua awamu ya tatu ya mradi wa TASAF, amesema kiasi cha shilingi trilioni 2 zitatumika kutoa ruzuku kwa kaya masikini, huku miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya na miundombinu zikiboreshwa ili kuimarisha kiwango cha hali ya maisha.

Hali ya umasiki inaripotiwa kuzidi  kuongezeka katika maeneo ya vijijini Tanzania

Tansania Nyumba Ntobhu
Picha: M. Meloni

Hata hivyo, ripoti ya maendeleo ya binadamu ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, iliyozinduliwa mwishoni mwaka uliopita, inaonesha kwa ujumla maendeleo yamerudi nyuma kwa asilimia 24.9 ilinganishwa na mwaka uliopita.

Lakini katika uchambuzi wa ripoti hiyo iliyozingatia hali ya kutokuwepo usawa katika mazingira ya kipato, elimu na utofauti wa walio na mali na wasio kuwa nazo, Tanzania bado inaonekana kuwa juu kimakadirio.

Dokta Albina Chuwa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu anasema uchambuzi wa takwimu unaonesha taifa hilo lina kasi katika kupambana na umasikini

Mpango huu wa TASAF, ambao unatumia matrilioni ya shilingi za Kitanzania zinazotolewa na wadau wa maendeleo, unatajwa kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya kaya kukosa sifa za kunufaika na mpango huo licha ya kupokea ruzuku. 

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wana matumaini kwamba endapo mpango wa kunusuru kaya masikini utaongeza kiwango cha ruzuku katika kaya, utasaidia taifa hili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2030.

Chanzo: Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam