1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania na Zambia kuimarisha uhusiano wa ujirani mwema

2 Agosti 2022

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia wamekubaliana maeneo saba ya ushirikiano ikiwemo kuimarisha uhusiano wa ujirani mwema kama ulivyohimizwa na waasisi wa mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/4F1TB
Dokumentation | Die Tazara - Mit dem Zug von Tansania nach Sambia
Picha: Autentic

Makubaliano hayo yamefikiwa Jumanne ikulu jijini Dar es Salaam ambako Rais Hichilema ameanza ziara ya siku mbili ya kiserikali. Wakizitambua hekima za waasisi wa mataifa hayo mawali, Mwalimu Julius Nyerere rais wa kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa na mwenzie Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda, marais hao wa sasa wanaona kwamba kuna wakati uhusiano wa kidugu wa pande hizo mbili ulipitia katika nyakati za milima na mabonde, lakini wakati umefika wa kuzienzi fikra za waasisi wake.

Rais Samia aliyekuwa wa kwanza kuzungumza aligusia kiini cha makubaliano hayo ikiwamo kurejesha upya uhusiano wa kidugu hasa kwa kutambua kwamba raia wa pande zote mbili wamekuwa wakiingilia karibu kila uchao kupitia eneo la Tunduma kwa upande wa Tanzania na lile la Nakonde upande wa Zambia.

Wakuu hao wa nchi waliokuwa wameambatana na mawaziri pamoja na maafisa wengine kwenye majadiliano hayo, wameafikiana kupanua ushirikiano kwenye sekta ya usalama na mkazo ukiwekwa zaidi katika eneo la kukabiliana na vitendo vya kigaidi.

Uimarishaji wa sekta ya miundombinu kupitia reli ya TAZARA ni eneo lingine ambalo wakuu hao wa nchi wanaona linapaswa kupewa msukumo na Rais Samia anasema jambo linalopaswa kutupiwa macho ni kuona reli hiyo inaboreshwa kufikia viwango vya kisasa.

Kwa upande wake Rais Hichilema anasema Tanzania na Zambia ni mataifa ndugu yanayopaswa kuendelea kunufaishana katika sekta za kijamii na biashara. Anasema hakuna haja kwa pande hizo kuendelea kutoleana macho bali kinachopaswa ni kuendelea kuilinda misingi iiyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo mawili na hilo litafanikiwa kwa kuendelea kufungua milango ya fursa kwa wananchi wa pande zote.

Tanzania na Zambia mataifa ambayo pia yamepitiwa na Ziwa Tanganyika wakati fulani yalijikuta yakiingia katika hali ya sintofahamu baada ya madereva wa malori wa Tanzania kupigwa marufuku kuingia nchini Zambia, mzozo ambao hata hivyo baadaye ulitafutiwa ufumbuzi.