1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TAMWA yaadhimisha miaka 36 tangu kuasisiwa

29 Novemba 2023

Chama cha Waandishi Habari Wanawake nchini Tanzania, TAMWA leo kinaadhimisha miaka 36 tangu kuasisiwa kwake kwa kuandaa makongamano juu ya hali ya uandishi habari nchini Tanzania.

https://p.dw.com/p/4ZZYX
Tansania Daressalam Media Women´s  Association TAMWA Jenista Mhagama
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama aliyemwakilisha Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akizungumza katika maadhimisho ya miaka 36 ya TAMWA.Picha: Florence Majani/DW

Chama cha Waandishi Habari Wanawake nchini Tanzania, TAMWA leo kinaadhimisha miaka 36 tangu kuasisiwa kwake huku kukiendeshwa makongamano yenye mijadala inayoakisi hali ya uandishi wa habari nchini humo.

Chama hicho kinasema kimepiga hatua kubwa katika kuwapigania waandishi wa habari wanawake waliopitia madhila makubwa ikiwamo kukumbana na vikwazo vya kiuchumi na kijinsia.

Hali ya uhuru wa vyombo vya habari ikoje nchini mwako?

Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe amesema hayo ni mafanikio makubwa hasa kwa kuzingatia historia ya uanzishwaji wake uliokuwa umegubigwa na mifumo dume mingi.

Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho haya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema anatambua mchango unaotolewa na waandishi wa habari wanawake.