1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waafghan 400 waliohamishwa wafikishwa Korea Kusini

26 Agosti 2021

Takriban raia 400 wa Afghanistan waliohamishwa wamewasili nchini Korea Kusini ambapo serikali ya nchi hiyo imesema inafanyia sheria marekebisho kuwaruhusu Waafghani waliofanya kazi nao kukaa nchini humo kwa muda mrefu

https://p.dw.com/p/3zVr8
Afghanistan | Evakuierungsflüge vom Flughafen Kabul
Picha: Yonhap/picture alliance

Angalau ndege mbili zilitarajiwa kuwasafirisha watu 391 wanaozijumuisha familia za wafanyakazi wa ubalozi wa Korea, taasisi ya ushirikiano wa kimataifa ya Korea KOICA, hospitali na taasisi ya mafunzo ya ufundi inayoendeshwa na serikali pamoja na ngome za kijeshi. Waziri wa sheria Park Beom-kye amesema kuwa raia wengi wa Korea Kusini walipokea usaidizi wa kimataifa baada ya kulazimika kutoroka vita nchini humo vya mwaka 1950 to 1953. Kabla ya kuwasili kwa ndege hizo, Beom-kye aliwahutubia waandishi habari nje ya uwanja wa ndege wa Incheon na kusema kuwa sasa ni wakati wa nchi hiyo kurudisha hisani. Beom-Kye alikiri utata unaozunguka mpango huo na kusema uamuzi wa kuwakubali wakimbizi kutoka Afghanistan ulikuwa mgumu lakini akaongeza kuwaKorea Kusini haiwezi kuwatelekeza rafiki zake.

Südkorea Präsident Moon Jae-in
Moon Jae-in - Rais wa Korea KusiniPicha: Jeon Heon-Kyun/REUTERS

Huku hayo yakijiri, maelfu ya raia wa Afghanistan leo walijaribu kuondoka nchini humo kupitia njia mbali mbali za barabara kufuatia hali isiyoeleweka ya kisiasa nchini mwao. Baadhi ya familia zilionekana zikijaribu kuingia Pakistan kupitia mpaka wake wa Kusini Magharibi wa Chaman. Mmoja wa watu hao Nasratullah Khan, aliyekimbia makazi yake huko Jalalabad karibu na Kabul katika eneo la Kaskazini, alisema kuwa alikuja njia yote hadi katika mpaka huo wa Chaman kwa sababu alifikiri itakuwa rahisi kuvuka mpaka huo kuliko ule wa Torkham.

Mataifa ya Magharibi yatoa onyo la mashambulio

Hapo jana usiku, onyo jipya lilitolewa kutoka mataifa ya Magharibi kuhusu uwezakano wa mashambulizi kutoka kwa tawi la kundi linalojiita dola la kiislamu IS nchini Afghanistan ambalo kuna uwezakano kwamba limeona kuimarika kwake kutokana na hatua ya kundi la Taliban kuwaachia huru wafungwa nchini humo. Tayari ndege za kijeshi za mizigo zinazoondoka katika uwanja wa ndege wa Kabul zimerusha ndimi za moto kuchanganya uwezekano wowote wa kulengwa kwa makombora huku wanajeshi wanaotoroka wakiacha nyuma silaha zao nzito na vifaa kote nchini humo kufuatia hatua ya Marekani ya kuondoa wanajeshi wake.

Waziri wa jeshi la Uingereza James Heappey leo ameliambia shirika la habari la nchi hiyo BBC kwamba kuna ripoti ya kuaminika ya uwezekano wa shambaulio  katika uwanja huo wa ndege katika masaa yajayo.