Tajani kuliongoza Bunge la Umoja wa Ulaya
18 Januari 2017Antonio Tajani, mshirika wa Waziri Mkuu wa zamani wa Italia Silvio Berlusconi, anachukua nafasi ya Martin Schulz kutoka Ujerumani, aliyemaliza muda wake. Tajani anayetoka katika muungano wa vyama vya kihafidhina vinavyofuata siasa za wastani za mrengo wa kulia wa European People's Party, EPP alimshinda kwa kura 351 Muitaliano mwenzake, Gianni Pitella kutoka muungano wa vyama vya siasa za wastani za mrengo wa kushoto vya kisoshalisti na kiliberali, S&D aliyepata kura 282.
Kura 633 zilikuwa halali kati ya jumla ya kura 713 zilizopigwa katika duru ya mwisho ya uchaguzi, huku wabunge 80 wakiwa hawajapiga kura. Akizungumza baada ya ushindi huo, Tajani ambaye amekuwa mjumbe wa bunge la Umoja wa Ulaya tangu mwaka 1994 ameahidi kutetea demokrasia na uhuru wa wananchi wa Umoja wa Ulaya.
''Huu ulikuwa mchakato wa kidemokrasia na kama nilivyosema leo, nitakuwa rais wa wote, nitamuheshimu kila mwakilishi na nitayaheshimu makundi yote,'' amesema Tajani.
Ahadi alizotoa
Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63, anajulikana kutokana na aina yake ya uwazi na washirika wengi, pamoja na ukaribu wake na Berlusconi. Aidha, ameahidi kupambana na ugaidi na kushughulikia masuala ya uhamiaji ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na wanasiasa wa mrengo wa kulia.
Kwa upande wa wanasiasa wa kijani, ameahidi kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na kwa wale wa mrengo wa kushoto amewaahidi kushughulikia suala la ukosefu wa ajira. Amebainisha kuwa uhuru ni jambo muhimu kwa Umoja wa Ulaya, muhimu kwa historia na mustakabali wa umoja huo.
Rais anayemaliza muda wake, Martin Schulz, amempongeza Tajani baada ya kuchaguliwa na amemtakia kila la heri katika majukumu yake mapya. Amesema yuko tayari kushirikiana naye kwa sababu Umoja wa Ulaya unahitaji bunge lenge nguvu na madhubuti.
Tangu mwaka 2014, Tajani ambaye pia ni mwanasheria, amekuwa makamu wa rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Pia amewahi kufanya kazi katika Halmashauri ya Umoja wa Ulaya. Kuanzia mwaka 2008 hadi 2010 alikuwa kamishna wa usafiri na kisha kuwa kamishna wa viwanda kuanzia mwaka 2010 hadi 2014.
Majukumu ya rais wa Bunge la Umoja wa Ulaya ni pamoja na kuangalia bajeti na shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria na kuhakikisha taratibu za bunge zinafanyika vizuri. Rais pia analiwakilisha bunge hilo katika masuala ya kimataifa na katika migogoro ya aina yoyote ile ya kisheria.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AFp, DPA
Mhariri: Caro Robi