Suala la Ukraine latawala mkutano wa mawaziri wa nje wa G20
21 Februari 2025Rais Cyril Ramaphosa aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuufungua mkutano huo jana Alhamisi kwamba hatua ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio ya kutoshiriki kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 nchini humo haikuwa ni ya kususia. Rubio alitangaza mapema mwezi huu kwamba hatashiriki mazungumzo ya wanadipomasia hao wa G20 kwa sababu mwenyeji wa mkutano ni mpinzani wa ajenda za Marekani.
Marekani badala yake iliwasilishwa na kaimu balozi wake mjini Pretoria, Dana Brown.
Ramaphosa amesisitiza kwamba "Kutokuwepo kwa baadhi ya viongozi sio mwisho wa dunia," na kuongeza kuwa ana imani mchakato wa kidiplomasia ndio pekee utaweza kubadilisha hali ya mambo katika uhusiano baina ya mataifa hayo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent pia alitangaza jana Alhamisi kwamba hatahudhuria mkutano wa G20 wa mawaziri wa Fedha na magavana wa Benki Kuu utakaofanyika Cape Town wiki ijayo.
Soma pia:Mawaziri wa kigeni wa G20 wakutana Afrika Kusini bila Marekani
Afrika Kusini, mwenyeji wa mazungumzo hayo kwa mwaka huu, imejikuta katika aina fulani ya makabiliano na Marekani na hasa kufuatia hatua yake ya kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ, ikiishutumu Israel kwa kufanya "mauaji ya halaiki" katika mashambulizi yake kwenye Ukanda wa Gaza, madai ambayo Israel imeyakanusha.
Lavrov ahudhuria mkutano, akutana na Wang Yi wa China
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amehudhuria mkutano huo baada ya mazungumzo ya kihistoria kati ya Marekani na Urusi wiki hii ya kumaliza vita nchini Ukraine, vinavyotimiza miaka mitatu wiki ijayo.
So,a pia:Kwa nini Marekani inaiadhibu Afrika Kusini kwa kuifutia misaada?
Lavrov alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi pembezoni mwa mkutano huo na kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Lavrov alisema mahusiano baina ya mataifa hayo mawili "yamezidi kuimarika na kubakia kama kigezo muhimu katika kuleta utulivu wa kimataifa.
Yi kwa upande wake ameuambia mkutano huo wa G20 kwamba anaunga mkono juhudi zote za kuleta amani nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Marekani na Urusi. Amesema China iko tayari kuchukua jukumu muhimu katika suluhu ya kisiasa, itakayojikita katika mahitaji ya pande zinazozozana lakini pia wasiwasi wa jumuiya ya kimataifa.
Katika hatua nyingine, Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas, alizungumzia matamshi ya Rais Donald Trump aliyemtaja Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kuwa dikteta, akisema alidhani Trump amemchanganya Zelensky na Rais Vladimir Putin wa Urusi, kwa kuwa ni wazi kiongozi huyo wa Urusi ndio dikteta.
Amewaambia waandishi wa habari mjini Johannesburg baada ya kuhudhuria mkutano huo wa G20 kwamba Zelensky ni kiongozi aliyechaguliwa kwenye uchaguzi huru na wa haki na kuongeza kuwa katiba za mataifa mengi zinaruhusu kusitishwa uchaguzi katika kipindi cha vita ili kujikita kwenye mzozo. Amesema lengo kuu kwa sasa linapaswa kubaki katika kuunga mkono Ukraine na kuiweka Urusi shinikizo zaidi la kisiasa na kiuchumi.
Wakati Afrika Kusini, inayoshikilia urais wa G20 mwaka huu, ikiwa na matumaini kwamba mkutano mkuu wa kwanza mkubwa wa kundi hilo utaleta mabadiliko kwenye maswala yanayoathiri mataifa yanayoendelea kama madeni na mabadiliko ya tabianchi, lakini maafisa wamesema majadiliano ya awali yalijikita kwenye hali ya kisiasa ulimwenguni.