1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Magharibi zilikuwa na mipango kutuvamia-Putin

9 Mei 2022

Rais Vladmir Putin wa Urusi amesema vikosi vya wanajeshi wake nchini Ukraine vinaitetea nchi yao dhidi ya kitisho kisichokubalika.

https://p.dw.com/p/4B1K4
Russland | Militärparade am 9. Mai in Moskau
Picha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Ni moja ya kauli alizotowa muda mfupi uliopita wakati akifungua gwaride la maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya ushindi katika vita vya pili vya dunia dhidi ya utawala wa wanazi wa Ujerumani.

Leo Jumatatu 09.05.2022 ni kumbukumbu ya miaka 77 ya maadhimisho  tangu ushindi  wa Urusi katika vita vya pili vya dunia dhidi ya wanazi wa Ujerumani na gwaride la maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka. Mbele ya maelfu ya wanajeshi wa Urusi katika uwanja wa kale wa kihistoria katika mji mkuu Moscow, wa Red Square rais Vladmir Putin amesema vikosi vya nchi hiyo vilivyoko ndani ya Ukraine vinaendelea na vita dhidi ya Unazi.

"Katika kipindi hiki mko vitani kwa ajili ya kuwapigania watoto wetu katika jimbo la Donbas, kwa ajili ya usalama wa nchi yetu Urusi.''

Putin amekwenda mbali na kuongeza kusema kwamba ni muhimu zaidi Urusi kufanya kila inachoweza  kumaliza uovu wa vita duniani na kuhakikisha hautokei tena.Ingawa pia hakutowa tangazo lolote kubwa kwenye hotuba yake licha ya kuwepo ripoti kwenye nchi za Magharibi kwamba huenda angetumia nafasi hiyo kutangaza kutanua vita hiyo ya Ukraine au kukusanya wanajeshi nchini Urusi.

Russland | Militärparade am 9. Mai in Moskau
Picha: Alexander Nemenov/AFP/Getty Images

Badala yake alijikita zaidi kwenye kutafuta uungwaji mkono wa umma wa kamepeini hii ya vita kwa kufungamanisha mgogoro huu na kile warusi wanachokiita vita vikubwa vya kizalendo. Aidha kiongozi huyo wa Urusi ameilaumu Ukraine na nchi za Magharibi kwa kusababisha vita hivyo akisema serikali ya kiev na washirika wake walikuwa wakijiandaa muda mrefu kuvamia maeneo yake ya kihistoria ikiwemo jimbo la Donbass na Crimea.

"Licha ya kuwepo mivutano ya kimataifa siku zote Urusi ilikuwa ikipigania kuundwa kwa mfumo wa usalama wenye kuzingatia usawa na usioleta migawanyiko, jambo ambalo ni muhimu kwa jumuiya yote ya kimataifa. Nchi za Jumuiya ya kujihami ya NATO hazikutaka kutusikiliza sisi maana yake ni kwamba, bila shaka walikuwa na mipango yao tafauti kabisa. Kitisho cha wazi kisichokubalika kwa usalama wetu kilitengenezwa na zaidi ya yote kililetwa moja kwa moja kwenye mipaka yetu''

Russland | Militärparade am 9. Mai in Moskau
Picha: Mikhail Metzel/SNA/IMAGO

Urusi ilikuwa haina budi bali kuchukua hatua ya kuzima uchokozi huo ameongeza kusema Rais Vladmir Putin na kusisitiza kwamba ulikuwa uamuzi pekee sahihi kuchukua kulinda mamlaka na uhuru wa nchi yake. Waziri wa ulinzi wa Uingereza ametoa kauli kuhusu kilichosemwa na Putin. Ben Wallace amesema Putin na majenerali wake wanaakisi ufashisti na utawala wa maovu ya ukatili ulioshuhudiwa miaka 77 iliyopita na uvamizi wake Ukraine hauheshimu historia yake ya kijeshi.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW