1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la kundi la Taliban lawajeruhi watu 95, Kabul

Sylvia Mwehozi
7 Agosti 2019

Serikali nchini Afghanistan imesema mlipuaji wa kujitoa mhanga amelipua bomu ndani ya gari siku ya Jumatano na kuwajeruhi watu 95. Mlipuaji wa kujitoa mhanga alilipua bomu lililotegwa ndani ya gari.

https://p.dw.com/p/3NUcp
Afghanistan Anschlag in Ghazni
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Nikzad

Shambulizi hilo limesababisha mlipuko mkubwa ambao umewajeruhi mamia ya watu. Kundi la Taliban limekiri kuhusika katika shambulizi hilo. Hakukuwa na uthibitisho wa mara moja kuhusu vifo vyovyote katika shambulizi hilo la pili katika mji huo mkuu wa Afghanistan katika muda wa siku chache zilizopita.

Msemaji wa polisi Firdaus Faramarz ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mlipuaji huyo, alilipua bomu hilo nje ya makao makuu ya polisi.

Taliban wadai kuhusika

Kundi la Taliban limesema kuwa lilikuwa limelenga kituo cha kuwasajili maafisa wa vikosi vya usalama kilichopo katika eneo hilo. Vyombo vya habari nchini humo vilionyesha moshi mkubwa ukitanda katika eneo la Kabul ambalo ni makazi ya jamii ya walio wachache ya Hazara.

Afghanistan Peace Talks Afghanistan Loya Jirga Kabul Ashraf Ghani
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani Picha: Reuters/O. Sobhani

Makao hayo makuu ya polisi yamelengwa katika siku zilizopita ikiwa ni pamoja na shambulizi la mwaka 2017 lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 20. Afisa mtendaji mkuu wa serikali Abdullah Abdullah amelaani shambulizi hilo na katika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter amesema kuwa lengo la magaidi hao ni kutatiza kampeini za uchaguzi wa urais.

Uchaguzi wa urais nchini Afghanistan ambao tayari umechelewa kutokana na sababu za usalama, unatarajiwa kufanyika tarehe 28 mwezi Septemba.

Siku ya Jumanne kundi la Taliban lilitoa onyo kwa raia wa Afghanistan kutoshiriki katika uchaguzi huo na kujiepusha na mikutano ya kampeini za uchaguzi ambayo huenda ikalengwa .

Kundi hilo ambalo limekuwa likitekeleza mashambulizi ya karibu kila siku nchini Afghanistan, kwa kawaida hulenga vikosi vya kijeshi vya serikali na maafisa wa serikali ama wale wanaoonekana kuegemea upande wa serikali.

Hakujawa utengamano nchini Afghanistan hata baada ya kundi la Taliban na Marekani kuonekana kuwa karibu kufikia mkataba wa kihistoria wa Marekani kuondoa vikosi vyake vya kijeshi ili kundihilo liweze kuweka ahadi kuwa nchi hiyo haitatumiwa kama ngome ya kupanga mashambulizi ya wanamgambo.