1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Burundi: Nkurunziza hakufa kutokana na corona

Zainab Aziz/ Eric Topona10 Juni 2020

Serikali ya Burundi imeeleza rasmi kwamba kifo cha rais Pierre Nkurunziza kilisababishwa na ugonjwa wa moyo. Lakini baadhi ya wachunguzi wanasema kwamba kiongozi huyo amekufa kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

https://p.dw.com/p/3dZ5U
Burundi Pierre Nkurunziza
Picha: picture-alliance/dpa/C. Karaba

Msemaji wa serikali ya Burundi ameiambia DW  kwamba rais huyo amekufa kutokana na maradhi ya moyo. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari kadhaa kiongozi huyo alipelekwa hospitali ya jimbo la Karuzi mwishoni mwa wiki liyopita.

Kwanza alipata afueni lakini hapo Jumatatu hali yake iligeuka na kuzidi kuwa mbaya. Nkurunziza alikufa akiwa na umri wa miaka 55. Mke wake alipelekwa Kenya jumatatu  hiyo hiyo kwa ajili ya matibabu ya corona.

Nkurunziza amekufa wakati rais mtuele Evariste Ndayishimiye anatarajiwa kuapishwa rasmi kushika  madaraka wiki chache zizajo. Ndayishimiye alishinda uchaguzi wa rais nchini Burundi mwezi uliopita baada  ya Nkurunziza kuamua kutogombea muhula mwingine.

Makamu wa rais Burundi azungumza juu ya kifo cha Nkurunziza

Kifo cha Nkurunziza chaitikisa Burundi

Kifo chake ni kama tetemeko la ardhi nchini  Burundi baada ya kuitawala nchi hiyo kwa muda  wa  miaka 15. Wachambuzi wanasema sasa Burundi  haiwezi tena kuficha ukweli juu ya janga la corona baada ya kifo cha kiongozi huyo na baada ya mke  wake kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu ya maradhi hayo!

Burundi yatangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa

Hapo awali wachambuzi walitarajia kumwona Nkurunziza akivuta hatamu za uongozi nyuma ya kiongozi mpya Ndayishimiye. Mtaalamu wa masuala  ya  Burundi Thierry Vircoulon amesema huenda kifo cha Nkurunziza kimetokana na mkakati wa kisiasa.

" Rais mpya anaetokea kwenye utawala wa  zamani sasa atakuwa na uwanja huru!" Amesema Thierry Vircoulon.

Rais Nkurunziza amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55.
Rais Nkurunziza amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55.Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Wasifu wa Nkurunziza

Nkurunziza aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu nchini Burundi alikuwa kiongozi wa waasi katika miaka ya nyuma. Mnamo mwaka 2015 aligombea muhula wa tatu wa rais na miaka mitatu baadae alibadilisha katiba ya Burundi kwa njia ya kura ya maoni ambayo ingemwezesha kutawala hadi mwaka 2034.

Tangu aingie madarakani watu zaidi ya 400,000 waliikimbia Burundi na maelfu wameuawa. Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague inafanya uchunguzi juu ya kukiukwa haki za binadamu wakati wa utawala wa Nkurunziza.