1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la See-Watch laapa litaendelea kuwaokoa wahamiaji

Angela Mdungu
2 Julai 2019

Shirika lisilo la kiserikali la Sea-Watch limesema litaendelea kuwaokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania hata kwa kutumia meli mpya ikibidi.

https://p.dw.com/p/3LTYB
Sea-Watch 3 Schiff - Handout von Sea-Watch
Picha: picture-alliance/dpa/Sea-Watch.org/C. Grodotzki

Kauli ya Sea watch imetolewa wakati Nahodha wake Carola Rackete akisubiri hukumu nchiniItalia baada ya kuwekwa kizuizini kwa kosa la kutia nanga katika bandari moja ya nchi hiyo bila idhini.

Rakeckete mwenye umri wa miaka 31, alikamatwa mwishoni mwa juma katika bandari ya kisiwa cha Lampedusa huko Italia na anadaiwa kuwa alifanya mawasiliano hafifu na boti za mamlaka ya forodha za nchi hiyo. Baada ya kukamatwa, Rackete alihojiwa kwa saa tatu katika mji wa Agrigento kwa tuhuma za kukataa kutii amri za meli ya jeshi na afisa wa umma. Mwanasheria wake Leornado Marino, aliliambia shirika la habari la DPA kuwa Rackete aliutetea uamuzi wake kwa kuwaambia mahakimu kuwa hali ndani ya boti ilikuwa mbaya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo salvini anayejulikana kwa msimamo wake ulio dhidi ya wahamiaji, amekuwa akizuia boti za uokoaji zinazosaidia wakimbizi kwa madai kuwa zinashirikiana na walanguzi wanaowasafirisha wahamiaji kwa njia haramu. Hata hivyo mwendesha mashitaka wa Sicily, ambaye anashiriki katika upelelezi wa kesi ya Rackete, Luigi Patronagio, amesema hawana uthibitisho wowote kuwa walanguzi  hao wanashirikiana na mashirika ya msaada ya uokoaji. 

See-Watch yaapa kuendelea kuwaokoa wahamiaji

Kwa upande wake asasi isiyo ya kiserikali ya Sea-Watch ambayo Rackete anaitumikia, imeapa kuendelea kuwaokoa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterania hata kwa kutumia meli mpya iitwayo See watch namba tatu kama watalazimika kufanya hivyo. Shirika hilo limesema, litaendelea kuheshimu haki za binadamu katika bahari hiyo.

Italien Kapitänin Carola Rackete
Nahodha Carola Rackete wa meli ya meli ya Sea-WatchPicha: Reuters/G. Mangiapane

Iwapo nahodha huyo atakutwa na hatia, huenda akakabiliwa na adhabu ya faini kubwa kwa mujibu wa sheria mpya ya Italia inayotaja adhabu kwa meli za kuwaokoa wahamiaji zisizo na idhini ya kuingia katika eneo la nchi hiyo.

Hata hivyo, shirika la Sea-Watch limesema linahofia kuwa kuwekwa kizuizini kwa Rackete kutasababisha vifo vya wahamiaji wengi zaidi kwenye bahari ya Mediterania kwani huenda manahodha wa meli zote wakaanza kujiuliza mara mbili iwapo wawaokoe wahamiaji ama la.

Naye msemaji wa kamisheni wa kamisheni ya Ulaya alipoulizwa kuzungumzia kisa cha kushikiliwa kwa Rackete alikataa kulizungumzia akidai kuwa kamisheni hiyo haina weledi wa kulishughulikia suala hilo. Kamisheni hiyo inasaidia kufanya majadiliano ya namna ya kugawana wahamiaji kwa nchi wanachama.