1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schulz ateuliwa kugombea ukansela kupitia SPD

29 Januari 2017

Rais wa zamani wa bunge la Ulaya, Martin Schulz, ameteuliwa kukiongoza chama cha Social Democratic katika jaribio lao la kumuondowa madarakani Kansela Angela Merkel.

https://p.dw.com/p/2Wb2d
Martin Schulz
Picha: Reuters/H. Hanschke

Rais wa zamani wa bunge la Ulaya, Martin Schulz, ameteuliwa kukiongoza chama cha Social Democratic katika jaribio lao la kumuondowa madarakani Kansela Angela Merkel na amesema atapigania kuwapo kwa usawa zaidi na kuondokana na mgawanyiko nchini Ujerumani.

Schulz ameuambia umma wa zaidi ya watu 1,000 katika makao makuu ya chama hicho mjini Berlin Jumapili (29.01.2016 )kwamba atapigania kuwepo kwa taratibu za kodi zitakazozingatia haki zaidi na kuhakikisha kwamba watu walioko katika maeneo ya vijijini wananufaika na mafao sawa na wenzao walioko katika miji mkubwa.

Pia ametowa wito wa kuwepo kwa mshikamano zaidi barani Ulaya katika suala la uhamiaji na kuvielezea vitendo vya Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, kuwa ni "tusi" kwa Umoja wa Ulaya.

Shulz amesema atavitaka vyama vyote kufikia makubaliano kuzuwiya aina ya kejeli zilozokuwa zimeshuhudiwa wakati wa kampeni za uchahuzi wa rais nchini Marekani mwaka jana.

Kutokwepa midahalo na wanasiasa wapinzani

SPD Kanzlerkandidat Martin Schulz
Martin Schulz akiwahutubia wanachama wa SPD Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Shulz ambaye aliwahi kuwa meya wa kutoka mji mdogo Ujerumani ya magharibi kabla ya kuwa rais wa Bunge la Ulaya amesema hatokwepa midahalo na wapinzani wake wa kisiasa lakini habari bandia kuhusu wagombea na kueneza ujumbe wa uzushi kwenye mitandao ya kijamii inabidi kukomeshwe.

"Kile tulichoshuhudia mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi nchini Marekani ,ukosefu wa heshima jambo ambalo limenifadhaisha sana." Shulz ameuambia umma uliokuwa ukimsikiliza na kuongeza "jambo ambalo limeanzisha mgawanyiko na kuharibu mambo mengi nchini humo ambayo kuna wakati ilitetea uhuru na kuvumiliana.Hilo halipaswi kututokea sisi nchini Ujerumani."

Wajumbe wa kamati kuu ya chama cha Social Democratic wamekubaliana kwa kauli moja Jumapili kumteua Shulz kuwa amgombea wao kwa nafasi ya Ukansela wadhifa ambao tokea jadi umekuwa unakwenda kwa chama chenye kupata idadi kubwa ya kura katika uchaguzi mkuu.

Uamuzi huo wa kamati kuu inabidi uidhinishwe katika mkutano mkuu  wa chama uliopangwa kufanyika tarehe 19 mwezi wa Machi wakati Shulz mwenye umri wa miaka 61 pia anatarajiwa kuwa kiongozi wa chama.Kiongozi alieko sasa Sigmar Gabriel alijiuzulu bila ya kutarajiwa kutowa nafasi kwa Schulz wiki iliopita.

Umashuhuri wa Shulz wakaribiana na Merkel 

Deutschland Schulz: SPD will stärkste Kraft werden
Wanachama wa SPD wakimsikiliza Schulz.Picha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Uchunguzi wa maoni unauweka umashuhuri wa Schulz karibu na ule wa Kansela Merkel  ambaye anagombania muhula wa nne katikab uchaguzi uliopangwa kufanyika Septemba 24.

Mtoto huyo wa polisi kutoka Wuerselem karibu na mpaka wa Uholanzi, Shulz  alizungumzia wazi wazi juu ya kutumbukia kwake kwenye ulevi kufuatia jeraha lililokatisha maisha yake katika mchezo wa soka ambapo alikuwa akin'gara na kusema anashukuru na kuwa na fursa ya pili katika maisha yake.

Ameahidi kufanya kampeni kwa kupigania kuwepo kwa haki zaidi za kijamii na sera ya kutovumuliwa kabisa kwa uhalifu akimkariri kiongozi mwanzake wa chama aliyesema "Mimi ni mliberali lakini sio mpumbavu."

Katika hotuba yake Schulz pia ameshutumu kauli za Rais, Donald Trump, kuhusu wanawake na jamii za wachache kuwa za "kuchukiza na hatari " na kwamba hazikubaliki kabisa   huku akiahidi kupambana na sera kali za mrengo wa kulia dhidi ya wahamiaji ambazo zimekuwa zikikuzwa na chama cha kizalendo Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD) katika miaka ya hivi karibuni.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AP/Reuters/

Mhariri : Lilian Mtono