1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarungi: Watekaji walitaka Nywila ya simu yangu

13 Januari 2025

Mwanaharakati na kosoaji wa serikali ya Tanzania Maria Sarungi amesema watekaji waliomteka siku ya Jumapili, walimlazimisha atoe nywila ya simu yake akiamini walitaka kuingilia shughuli zake mitandaoni.

https://p.dw.com/p/4p7YU
Tanzania | Mwanaharakati Maria Sarungi Tsehai
Mwanaharakati na kosoaji wa serikali ya Tanzania Maria Sarungi Picha: Imani Nsamila

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwanaharakati na mtetezi wa haki za binadamu Maria Sarungi hakuwa na hofu yoyote na kusisitiza kuwa kamwe huu sio mwisho na wala hatokubali kunyamazishwa.

Maria Sarungi ambaye ni raia wa Tanzania anasimulia kuwa alikamatwa alipokuwa saluni akitengezwa nywele alipomuona dada mmoja ambaye alimshuku na ambaye hakumuelewa.

Soma pia:Mkosoaji wa serikali ya Tanzania aachiwa baada ya kutekwa nyara

Waliomteka walimkamata alipokuwa nje mtaani Kilimani na kumsweka kwenye gari jeusi aina ya Noah na kumfunika macho. Video iliyosambaa mtandaoni ililionyesha gari hilo la Noah likizuiliwa na matatu ya Citi Hopa. Kwa mtazamo wake, purukushani iliyozuka ndiyo iliyomuokoa.

"Mimi ni miongoni mwa watu wachache ambao hili tukio limetokea na nimepona, kuna wengi ambao wamepotea na bado wanapigiwa kelele Tanzania." Alisema mwanaharati huyo.

Aidha aliongeza kwamba miongoni mwa mambo ambayo watekaji hao walimshurutisha kufanya ni pamoja na kutoa simu yake jambo ambalo walifanikiwa na baadae kumlazimisha kutoa nywila ya simu.

"Naamini dhamira yao ilikuwa ni kupata vifaa vyangu kama simu na kuingia katika akaunti zangu za mitandaoni, ikiwa ni pamoja na kuchunguza shughuli zangu ninazozifanya huko.

Mwanaharakati huyo amesema kwamba wakati wanamuachilia walimuonya kuongea na yeyeote na kumsisitizia kuwa bado wanamfuatilia.

Amnesty International: utekaji unarudisha nyuma haki

Shirika La kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha mwanaharakati Maria Sarungi Tsehai anaachiliwa huru na akiwa salama.

Ebole ni mtafiti wa masuala ya haki ya Tanzania na Kenya kwenye shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International na anasisitiza vitendo hivyo vinarejesha nyuma haki.

Waandamanaji kadhaa watiwa mbaroni Kenya

Wakati huohuo, Tanzania inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka huu. Maria Sarungi Tsehai ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Samia Suluhu wa Tanzania na amekuwa Kenya tangu miaka 4 iliyopita pale hati ya kumkamata ilipotolewa na marehemu rais John Magufuli.

Nchini Kenya anamiliki televisheni ya dijitali inayoitwa Mwanzo. Kwenye mtandao wa X pekee, Maria ana wafuasi zaidi ya milioni 1.3. Kitendo cha kumteka nyara Maria Sarungi kimezua hisia mseto kwenye jamii ya kimataifa akiwemo mwakilishi mkaazi wa Umoja wa mataifa Stephen Jackson aliyetiwa tashwishi na hali hiyo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Kenya , Henriette Geiger alielezea tukio hilo kuwa la kutia wasiwasi. Hii ni mara ya pili kwa mwanaharakati wa Afrika Mashariki kutekwa katika mitaa ya kifahari mjini Nairobi ikiwa imepita miezi mitatu tangu kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye alipokamatwa na kurejeshwa kwao Uganda.

Soma pia:Mwanaharakati wa Tanzania Maria Sarungi asema yuko salama baada ya kutekwa nyara Nairobi

Kwa Kenya, watu wasiopungua 80 bado hawajulikani waliko tangu yalipofanyika maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa 2024 uliozua utata

Utekaji huo unazua maswali kuhusu msimamo wa Kenya ambayo inajiunga rasmi na baraza la haki la Umoja wa Mataifa mwezi huu wa Januari.