1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia Suluhu: Serikali si mshindani wa vyombo vya habari

18 Juni 2024

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amewaambia waandishi wa habari nchini humo kuwa serikali yake siyo mshindani wa vyombo vya habari bali inavitazama kama mbia wa karibu.

https://p.dw.com/p/4hCmf
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Ericky Boniphace/DW

Pia, amevitaka vyombo hivyo kufanya kazi kwa kufuata miiko ya kitaaluma huku vikizingatia kuweka mbele maslahi ya taifa. 

Rais Samia ambaye alikuwa akizungumza wakati akifungua kongamano ka siku mbili la maendeleo ya sekta ya habari linalofanyika jijini Dar es salaam, amewahakikishia waandishi wa habari kuwa utawala wake hauna haja ya kubinya vyombo vya habari na akawataka kuchapa kazi kwa uwazi na ukweli.

Alisema yeye ni muumini wa dhati wa uhuru wa maoni na kwa jinsi hiyo anavitazama vyombo hivyo vya habari kama mshirika wa karibu na serikali.

Kongamano hilo ambalo linafanyika kwa mara ya pili, linawaleta pamoja waandishi wa habari kutoka kada mbalimnali, ikiwamo wale wanaotoka taasisi za umma na zile binafsi. Wote kwa pamoja wanazijadili na kuzipa tafakuri changamoto na fursa zinazoizunguka sekta hiyo hasa katika nyakati hizi zinazoshuhudia mabadiliko ya kasi ya kidigitali.

Kufungiwa kwa Gazeti la Raia Mwema nchini Tanzania

Fursa kwa waandishi wa habari kusaka majawabu ya pamoja

Waziri wa habari, mawasiliano na teknolojia ya habari, Nape Nnauye alisema kongamano hilo ambalo pia limehudhuriwa na mabalozi, linatoa fursa kwa waandishi wa habari kusaka majawabu ya pamoja hasa kwa kuzingatia kuwa teknolojia imeifanya sekta ya habari kupitia katika mabadiliko.

Ama, amesema masuala mengine yanayohusu maendeleo ya habari kwa ujumla pamoja na dhima ya waandishi wa habari wakati huu wa kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani ni sehemu ya mijadala katika kongamano hilo.

Kongamano hilo pia linatazamiwa kujadili ripoti iliyozinduliwa Jumanne, ripoti ambayo inaangazia hali ya ustawi wa waandishi wa habari kitaaluma na kwa kipato.

Changamoto zinazoendelea kuikabili sekta ya habari

Ripoti hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati iliyoundwa kutathmini hali hiyo, Tido Mhando imeorodhesha changamoto zinazoendelea kuikabili sekta hiyo huku ikitaja sababu za kuendelea kuporomoka uchapishaji wa magezeti.

Mwanahalisia kushitaki serikali ya Tanzania

Viwango duni vya mishahara, kuanguka kwa soko la magazeti pamoja na malimbikizo ya madeni kutoka serikalini kumefanya ustawi wa vyombo vya habari nchini kuzidi kuporomoka. Kamati hiyo imependekeza kuchukuliwa hatua za haraka kunusuru hali hiyo, ikiwamo serikali kulipa madeni yake kwa vyombo vya habari.

Kongamano hilo linatazamiwa kutoa maazimio ya pamoja kuhusu mwenendo wa vyombo vya habari kuelekea siku za usoni hasa wakati huu dunia inapoingia katika enzi mpya ya matumizi ya akili ya kubuni.