1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda yatangaza waziri mpya wa mambo ya nje

13 Juni 2024

Rais Paul Kagame wa Rwanda amemteuwa waziri mpya wa mambo ya nje na mkuu wa ujasusi kabla ya uchaguzi. Kagame amemteuwa Olivier Nduhungirehe kuwa waziri wa mambo ya nje.

https://p.dw.com/p/4h0Es
Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Estácio Valoi/DW

Rwanda imemteuwa waziri mpya wa mambo ya kigeni na mkuu wa ujasusi katika mabadiliko yaliyofanywa mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa kitaifa ambao kiongozi wa muda mrefu Paul Kagame anatarajiwa na wengi kushinda.

Waziri Mkuu Edouard Ngirente amesema katika taarifa kuwa Olivier Nduhungirehe, ambaye zamani alikuwa balozi wa Rwanda nchini Uholanzi, ameteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje.

Anachukua nafasi ya mwanasiasa mkongwe Vincent Biruta, ambaye ametangazwa kuwa waziri wa mambo ya ndani.

Mwendesha mashitaka mkuu wa zamani Aimable Havugiyaremye pia ametangazwa kuwa katibu mkuu mpya wa Idara ya Ujasusi na Usalama wa Taifa, ikiwa ni mara ya kwanza kwa taasisi hiyo kuwa na kiongozi wa kiraia.

Anachukua nafasi ya Brigedia Jenerali Joseph Nzabamwita ambaye ameshikilia nafasi hiyo tangu mwaka wa 2016, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, na ambaye atakuwa mshauri mwandamizi wa usalama katika ofisi ya rais.

Rwanda inajiandaa kwa uchaguzi wa rais na bunge Julai 15.