1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto atangaza kuondoa marufuku ya biashara ya magogo

3 Julai 2023

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza kuondoa marufuku ya biashara ya magogo ya miti iliyodumu kwa takribani miaka sita licha ya ukosoaji kutoka kwa wanaharakati wa mazingira.

https://p.dw.com/p/4TLPD
Kenias Präsident William Ruto
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Kiongozi amesema uamuzi huo ni jambo "lililochelewa" na unalenga kuunda nafasi mpya za kazi na kuzifungua sekta za uchumi zinazotegemea misitu. Amesema ni jambo lisilokubalika kuiacha miti iliyokamaa ikiharibika misituni huku wakaazi wa maeneo hayo wakitaabika kwa kukosa mbao.

Ruto, ambaye amekuwa akijipigia upatu kuwa miongoni mwa viongozi walio mstari wa mbele barani Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, amesema ili kufidia ukataji wa magogo, serikali yake inalenga kupanda miti bilioni 15 katika muda miaka 10 inayokuja.

Soma zaidi: Rais William Ruto wa Kenya ameondoa marufuku ya ukataji miti kwenye misitu

Uamuzi wa kuruhusu tena biashara ya magogo yumkini utawavutia wafanyabiashara wa mbao ambao walipinga marufuku iliyowekwa mwaka 2018 na utawala uliotangulia. Hata hivyo, shirika la mazingira la Greepeace Africa limetahadharisha kwamba uamuzi huo utakuwa na taathira zisiso mfano kwa mazingira.