1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Russia, USA, zakubaliana kufikisha mwisho vita Ukraine

19 Februari 2025

Marekani na Urusi zimekubaliana kurejesha utendaji wa kawaida wa ofisi za kidiplomasia za kila upande, katika mabadiliko makubwa ya kisera tangu uvamizi wa Moscow nchini Ukraine uliopelekea kutengwa kwa Moscow.

https://p.dw.com/p/4qh8c
Urusi Riyadh 2025 | Mazungumzo kati ya Marekani na Urusi nchini Saudi Arabia kati ya Sergei Lavrov na Marco Rubio
Ujumbe wa Marekani na Urusi ukiwa katika mkutano pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal bin Farhan Al-Saud, Februari 18, 2025.Picha: Russian Foreign Ministry/Press S/picture alliance

Urusi na Marekani zimefikia makubaliano ya kuanza juhudi za kumaliza vita vya Ukraine na kuboresha mahusiano yao ya kidiplomasia na kiuchumi. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mazungumzo kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo mawili, hatua inayoashiria mabadiliko makubwa ya sera ya kigeni ya Marekani chini ya Rais Donald Trump.

Katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alisema pande zote mbili zimekubaliana kwa jumla kufanikisha malengo matatu makuu: kurejesha wafanyakazi wa kidiplomasia katika balozi zao jijini Washington na Moscow, kuunda timu ya ngazi ya juu kusaidia mazungumzo ya amani ya Ukraine, na kuchunguza fursa za kushirikiana kiuchumi na kidiplomasia.

Hata hivyo, Rubio alisisitiza kuwa mazungumzo haya ni mwanzo tu wa mazungumzo marefu yanayohitaji kazi zaidi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, alikubaliana na maoni haya na kusema kuwa mazungumzo yalikuwa ya "manufaa sana."

Mazungumzo haya yalihudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande zote mbili, akiwemo mshauri wa usalama wa taifa wa Trump, Michael Waltz, na mjumbe maalum wa Mashariki ya Kati, Steven Witkoff, huku Urusi ikiwasilishwa na mshauri wa mambo ya nje wa Rais Vladimir Putin, Yuri Ushakov.

Saudi Arabia | Mazungumzo kuhusu vita vya Ukraine mjini Riyadh
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, Msaidizi wa Rais Yuri Ushakov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Mshauri wa Usalama wa Taifa Michael Waltz (kutoka kushoto kwenda kulia katikati) wakizungumza wakati wa mapumziko katika mazungumzo ya pande mbili katika Kasri la Diriyah, Kijiji cha Al Basateen.Picha: Russian Foreign Ministry/TASS/dpa/picture alliance

Hata hivyo, hakuna afisa yeyote wa Ukraine aliyeshiriki mazungumzo hayo, jambo lililozua wasiwasi mkubwa kwa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, ambaye alitangaza kuwa nchi yake haitakubali matokeo yoyote ya mazungumzo hayo kwa kuwa haikushiriki. Zelenskyy pia aliahirisha ziara yake iliyopangwa kwenda Saudi Arabia.

Matarajio ya uboresha mahusiano ya kidiplomasia

Mahusiano kati ya Urusi na Marekani yamekuwa mabaya zaidi tangu Urusi ilipoikalia Crimea mwaka 2014, na hali ilizidi kuwa mbaya baada ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022. Mataifa ya Magharibi, ikiwemo Marekani, yameiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi kwa lengo la kuidhoofisha kiuchumi. Hali hiyo pia imesababisha kufukuzwa kwa idadi kubwa ya wanadiplomasia kutoka balozi za pande zote mbili.

Soma pia: Trump atangaza kukutana na Putin siku za usoni

Rubio alieleza kuwa kumaliza vita vya Ukraine kunaweza kufungua milango kwa ushirikiano mpana wa kiuchumi kati ya Marekani na Urusi. Matamshi haya yanadhihirisha mabadiliko makubwa katika sera ya Marekani kuhusu Urusi, hasa baada ya utawala wa Rais wa zamani Joe Biden kuongoza juhudi za kimataifa za kuiwekea vikwazo Moscow.

Mazungumzo haya pia yamepangiwa kuweka msingi wa mkutano wa kilele kati ya Rais Trump na Rais Putin, ingawa tarehe rasmi bado haijapangwa.

Hatua ya Marekani kuanza mazungumzo na Urusi imewafanya washirika wake wa Ulaya kuwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kupuuzwa katika juhudi za kusaka amani. Mnamo Jumatatu, Ufaransa iliitisha kikao cha dharura cha Umoja wa Ulaya kujadili hali ya Ukraine. Kwa mujibu wa sera ya awali ya Biden, Ukraine ilipaswa kuwa mshiriki wa mazungumzo yoyote kuhusu mustakabali wake.

Rubio alisema kuwa kumaliza mgogoro huu kutahitaji pande zote kufanya makubaliano, huku akisisitiza kuwa Ulaya pia ina nafasi muhimu katika mazungumzo haya, hasa kwa kuwa imeshiriki katika kuiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi.

Mwishoni mwa juma lililopita, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, alisema kuwa uanachama wa Ukraine katika NATO si jambo linalowezekana kwa sasa, na akapendekeza kuwa Kyiv inapaswa kuzingatia uwezekano wa kukubali upotevu wa baadhi ya maeneo yake kwa Urusi. Hii ni hoja inayokidhi matakwa makubwa ya Putin kuhusu mzozo huu.

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Juhudi za Saudi Arabia

Mazungumzo haya yalifanyika katika kasri la Diriyah jijini Riyadh, Saudi Arabia, na yanaonesha juhudi za Mwanamfalme Mohammed bin Salman kujiimarisha kama kiongozi wa kidiplomasia wa kimataifa. Saudi Arabia imekuwa na uhusiano wa karibu na Urusi, hasa kupitia ushirikiano wa kiuchumi kwenye kundi la OPEC+.

Soma pia:Mabadiliko ya kimataifa kuamua awamu mpya ya vita Ukraine 

Saudi Arabia pia imeshiriki katika majadiliano ya kubadilishana wafungwa wa vita kati ya Urusi na Ukraine. Hata hivyo, Zelenskyy aliahirisha ziara yake iliyopangwa kwenda Saudi Arabia wiki hii ili kuepuka kuhusishwa moja kwa moja na mazungumzo haya.

Licha ya juhudi za kidiplomasia, vita nchini Ukraine vinaendelea. Jeshi la anga la Ukraine lilisema kuwa Urusi ilirusha droni 176 usiku wa kuamkia Jumanne, ambapo nyingi ziliharibiwa kabla ya kufika malengo yake.

Hata hivyo, shambulizi moja liliathiri jengo la makazi katika mkoa wa Kirovohrad, na kujeruhi mama na watoto wake wawili, huku majengo mengine manne yakiharibiwa katika mkoa wa Cherkasy.

Hali ya mgogoro bado ni mbaya, na hatma ya makubaliano mapya kati ya Urusi na Marekani itaendelea kuangaliwa kwa karibu na mataifa mengine duniani.