1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ronaldo awajibu wakosoaji

19 Desemba 2016

Cristiano Ronaldo amesema amewajibu wakosoaji wake katika njia ya kipekee wakati aliukamilisha mwaka wa kuvutia zaidi kwa kufunga hatrick wakati Real Madrid ilishinda Kombe la Klabu bingwa Duniani

https://p.dw.com/p/2UXBI
FIFA Klub-Weltmeisterschaft  Finale  Real Madrid v Kashima Antlers  Toni Kroos
Picha: Getty Images/AFP/T. Yamanaka

Baada ya Madrid kuiangusha Kashima Antlers ya Japan kwa mabao manne kwa mawili baada ya kipindi cha muda wa ziada jana, nyota huyo wa Ureno aliukamilisha msimu wenye mafanikio makubwa ambao pia alinyanyua Kombe la Champions League, Super Cup, Euro 2016 na tuzo ya Ballon d'Or. CR7 alisema baada ya fainali hiyo kuwa "Umekuwa mwaka mzuri sana kwangu na umekamilika kwa njia hii, nna furaha kubwa. Ukiniuliza ni kombe lipi lililonifurahisha sana, ni ngumu kuchagua kwa sababu mataji yote ni tofauti, lakini Kombe la Ureno katika dimba la Ulaya ni maalum kwangu".

Ronaldo alionyesha ni kwa nini alipigiwakura ya kuwa mchezaji bora wa mwka kwa mara ya nne wiki iliyopita, katika fainali hiyo mbele ya mashabiki 68,000 uwanjani Yokohama. Na CR7 ambaye ana umri wa miaka 31 amesema bado ana kiu ya kushinda mataji zaidi.

Mfumo wa kutumia refarii wa video

FIFA Klub-Weltmeisterschaft Japan 2016 - Atletico Nacional vs. Kashima Antlers VIDEOBEWEIS
Refarii akiangalia picha za video kabla ya kufanya uamuziPicha: Reuters/K. Kyung-Hoon

Na tukibakia huko Japan, ni kuwa Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA limetoa tathmini yake ya mfumo wa kutumia video wakati wa mechi likisema ulikuwa mzuri sana. Mfumo wa kutumia video unajaribu kutafuta uungwaji mkono wakati teknolojia hiyo ilizusha utata katika mechi mbili za dimba hilo. Katika nusu fainali Real Madrid iliishinda Club America 2-0 na bao la Ronaldo katika dakika za majeruhi liliwakasirisha baadhi ya mashabiki. Kwanza lilifutwa kwa kuonekana kuotea lakini baadaye likakubaliwa baada kuangalia video.

Awali, mfumo huo wa video ulitumika kwa mara ya kwanza kwa kuruhusu penalty wakati Kashima Antlers iliifunga Atletico Nacional ya Colombia. Ilichukua muda kufikia uamuzi huo wa penalty hatua iliyowakasirisha mashabiki. Lakini rais wa FIFA Gianni Infantino anasema marefarii watastahili kuuzoea mfumo huo wakati utaanza kutumika "muhimu ni kuwa maamuzi yalikuwa sahihi. marefarii walifanya uamuzi sahihi na waliweza kusaidiwa na video. Lengo letu na imani yetu ni kuwa mfumo huu wa video unaweza kutumika kwa ajili ya manufaa makubwa, kitu ambacho ni muhimu katika mtiririko wa mechi.

Afisa Mkuu wa maendeleo ya teknolojia katika FIFA Marco van Basten anasema mfumo huo utakuwa bora zaidi wakati watanza kuuzoea "Wakati tunashirikiana na refarii anayetumia video, nadhani mambo yatakuwa bora kwa sababu tutakuwa na macho mengi yili kufanya uamuzi mzuri. Hivyo hata wakati labda kila kitu hakionekani kwa jicho, mwishowe matokeo yanaweza kuwa ya haki kwa sababu maamuzi yalikuwa sahihi".

Na mmoja ambaye anaunga mkono teknolojia hiyo ni kocha wa Barcelona Luis Enrique "naunga mkono mfumo wa video na kila kitu kinachoweza kuwasaidia marefarii. Mabadiliko ya kandanda yanapaswa kufuata mkondo huu. lakini ni muhimu kufafanua ni aina gani ya mchezo unapaswa kusimamishwa na ni muda gani unapaswa kutumiwa ili kuitathmini video".

Mwandishi: Bruce Amani/AP/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga