1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa amsimamisha kazi mkuu wa kupambana na ufisadi

10 Juni 2022

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amemsimamisha kazi mkuu wa ofisi ya kukabiliana na ufisadi siku moja tu baada ya mkuu huyo kuanzisha uchunguzi wa utakatishaji fedha dhidi ya rais huyo.

https://p.dw.com/p/4CWAt
Südafrika Besuch des Bundeskanzlers Olaf Scholz
Picha: Phill Magakoe/AFP

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Ramaphosa siku ya Ijumaa (10 Juni) ilisema: "Wakili Busisiwe Mkhwebane ataendelea kusimamishwa kazi hadi mchakato ulioanza kwenye Bunge utakapokamilika na nafasi yake inashikiliwa na naibu wake." 

Ofisi hiyo iliongeza kuwa kutokuwepo kwa Mkhwebane ofisini hakutazuwia uchunguzi wowote ambao ulianzishwa naye. 

Tangazo hilo lilikuja ikiwa ni siku moja tu tangu Mkhwebane aanzishe rasmi uchunguzi juu Rais Ramaphosa kuficha wizi uliofanyika kwenye nyumba yake ya shambani mwaka 2020.

Mahasimu wa Ramasphosa wanasema kashfa hiyo iliibuwa mpango mkubwa wa kutakatisha fedha unaofanywa na rais huyo, kwani wezi walioingia kwenye nyumba yake walikuta fedha taslimu dola milioni nne za Kimarekani zikiwa zimefichwa kwenye samani za nyumba hiyo.

Bunge lataka kumuondowa Mkhwebane

Südafrika Kapstadt | Brand im Parlament
Rais Cyril RamapahosaPicha: Sumaya Hisham/REUTERS

Bunge linalotawaliwa na chama cha Ramaphosa, ANC, lilianzisha mchakato wa kumuondowa kwenye nafasi yake mkuu huyo wa kupambana na ufisadi, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo na mtangulizi wa Ramaphosa, Jacob Zuma.

Kuteuliwa kwake Mkhwebane kulionekana na wengi kama jaribio la kulinda Zuma dhidi ya madai ya ufisadi. Kwa miaka kadhaa, amekuwa akifunguwa kesi na kushindwa akijaribu kuzuwia kuondoshwa kwenye nafasi yake.

Wakati Ramaphosa akitangaza kumsimamisha kazi Mkhwebane, kambi ya upinzani ilichachamaa bungeni hapo jana ikimtaka rais huyo ajiuzulu kupisha uchunguzi wa uhalifu dhidi yake kwa kuficha wizi huo uliofanyika nyumbani kwake.

EFF wataka Ramaphosa awawajibishwe

Ungarn Ernteraub Jugendliche
Kiongozi wa chama cha Economic Freedom FightersPicha: AP

Wabunge wa chama cha Economic Freedom Fighters waliondolewa kwa nguvu bungeni kwa kuingilia kila mara hotuba ya Ramaphosa alipokuwa akiwasilisha bajeti ya ofisi yake.

Mmoja wao, Natasha Ntlangwini, alisema kwa nguvu bungeni: "Hatuwezi kuhutubiwa na mtakatishaji fedha na mhalifu. Hatuwezi kuhutubiwa na mtu anayetuhumiwa kutenda makosa makubwa ya uhalifu." 

Wizi huo wa mwaka 2020 ulifanyika kwenye nyumba yake iliyo katika jimbo la kaskazini la Limpopo na kwa mara ya kwanza uliandikishwa mwezi huu na mkuu wa zamani wa ujasusi, Arthur Fraser.

Baadaye Ramaphosa alithibitisha juu ya wizi huo akisema kuwa fedha hizo dola milioni nne taslimu zilikuwa malipo aliyopata kwa kuuza wanyama kwenye kitalu chake. Alidai kuwa aliripoti kwa mkuu wa kikosi chake cha ulinzi lakini sio kwa polisi.