1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ramaphosa ala kiapo kuwa rais wa Afrika Kusini

Daniel Gakuba
25 Mei 2019

Cyril Ramaphosa amekula kiapo cha kuchukua muhula wa miaka mitano ya urais wa Afrika Kusini. Baada ya kuapishwa, Ramaphosa amesema Afrika Kusini inakabiliwa na changamoto kubwa, ambazo lakini zinaweza kupata suluhu.

https://p.dw.com/p/3J4So
Südafrika Pretoria | Amtseinführung Cyril Ramaphosa, Präsident
Picha: Reuters/S. Sibeko

Sherehe ya kuapishwa kwa Ramaphosa imehudhuriwa  na umati wa watu wapatao 30,000 waliofurika katika uwanja wa mpira mjini Pretoria. Ni baada ya ushindi wa chama chake cha African National Congress (ANC), wa asilimia 57 ya kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mapema mwezi huu wa Mei. Huo ulikuwa ushindi mdogo kabisa kwa chama hicho tangu kilipoingia madarakani mwaka 1994 baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Changamoto zinazomkabili 

Akihutubia baada ya kula kiapo, Cyril Ramaphosa amesema Afrika Kusini kama taifa inakabiliwa na changamoto ambazo ni dhahiri na nyingi. Hata hivyo ameongeza kuwa ''changamoto hizo zinaweza kutatuliwa, na nasimama mbele yenu kusema zitatafutiwa ufumbuzi.''

Südafrika Pretoria | Amtseinführung Cyril Ramaphosa, Präsident
Umati wa watu uliojitokeza katika sherehe za uapishoPicha: Reuters/S. Sibeko

Kiongozi huyo ametowa wito wa kuwepo nchi isio na wizi wala matumizi mabovu ya rasilimali za umma, akiwataka raia wa nchi hiyo kupambana kumaliza umaskini katika muda wa kizazi kimoja. Amesema ubadhirifu na uongozi mbaya vimeigharimu Afrika Kusini mabilioni ya rand, sarafu inayotumiwa nchini humo, na kukiri kuwa nchi hiyo ina pengo kubwa zaidi duniani la kipato baina ya matajiri na maskini.

Ramaphosa vile vile ameyazungumzia matatizo ya ukosefu wa ajira na huduma za kijamii zisizo za kuridhisha. ''Bado Waafrika Kusini wengi wanalala njaa, na wengi wanaishi katika umaskini wa kutupwa,'' amekiri na kuongeza kuwa inasikitisha kuwa vijana wengi hawana kazi.

Kibarua kikubwa kinachomsubiri Ramaphosani kuwavutia vijana waliozaliwa baada ya kumalizika kwa utawala dhalimu wa ubaguzi wa rangi, ambao tofauti na wazazi wao hawaichukulii ANC kama chama cha ukombozi, bali chama tawala kinachopaswa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za msingi.

Ramaphosa achukua mikoba ya Zuma

Cyril Ramaphosa alichukua madaraka ya urais baada ya rais aliyekuwepo, Jacob Zuma, kushurutishwa kuachia madaraka, alipozidiwa na shinikizo kuhusiana na mlolongo wa shutuma za ufisadi zilizokuwa zikimwandama.

Südafrika Pretoria | Amtseinführung Cyril Ramaphosa, Präsident
Shamra shamra za wafuasi wa RamaphosaPicha: Reuters/S. Sibeko

Wafuasi wengi wa ANC wanamuona Ramaphosa ambaye alikuwa mtu wa karibu wa rais wa kwanza mweusi, Nelson Mandela, kuwa na uwezo wa kukirudishia heshima chama chao. Mmoja wa viongozi waandamizi wa chama hicho, Fikile Mbalula amesema isingekuwa haiba ya Ramaphosa, ANC isingeweza kupata hata asilimia 40 ya kura katika uchaguzi uliopita.

Soma zaidi...

Mtangulizi wa Ramaphosa, Jacob Zuma ambaye anashikilia kuwa shutuma dhidi yake zina malengo ya kisiasa, hakuonekana katika sherehe za leo za kumwapisha rais. Washirika wa Zuma ni mahasimu wakubwa wa Ramaphosa na mipango yake ya kuleta mageuzi ndani ya ANC.