1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa zamani wa Italia Giorgio Napolitano aagwa

26 Septemba 2023

Italia imemuaga rais wa zamani Giorgio Napolitano na mazishi ya kitaifa leo Jumanne mjini Roma yaliyohudhuriwa na wanasiasa mashuhuri wa ndani na nje ya nchi akiwemo rais Sergio Mattarela na waziri mkuu Giorgia Meloni.

https://p.dw.com/p/4Wph2
Ehemaliger Staatspräsident Italien - 
Giorgio Napolitano
Picha: Italy Photo Press/IMAGO

Italia imefanya mazishi yake ya kwanza yasiyo ya kidini kwa kiongozi wa dola leo Jumanne ilipoanda ibada maalumu bungeni kumuaga rais wa zamani Giorgio Napolitano, aliyewahi mara mbili kuwa rais wa Italia aliyeaga dunia Ijumaa wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 98. Napolitano alikuwa mawanasiasa wa zamani mkomunisti kuwa rais na mtu wa kwanza kuchaguliwa mara mbili kwa wadhifa huo alioushikilia kati ya mwaka 2006 na 2015.

Rais wa Italia, Sergio Mattarela na waziri mkuu Giorgia Meloni wamehudhuria hafla ya kumuanga Napolitano.

Mtoto wa kiume wa Napolitano, Giulio, na mjukuu wake wa kike, Sophia, wametoa hotuba za hisia na kutoa heshima zao kwa kazi yake ya kisiasa. Sophia amesema, "Napolitano alikuwa mwanasiasa na kiongozi wa haiba kubwa, lakini pia alikuwa babu mwenye upendo na kuheshimika. Alikuwa mtu wa kujali, makini, na kila wakati alikuwepo kwa ajili yetu. Alisikiliza shida zetu na mahangaiko yetu kwa njia ya ushiriki na huruma na alijaribu wakati wote kutoa suluhisho, hata kama tayari alikuwa na shughuli nyingi akishughulikia matatizo yake, au niseme, matatizo ya nchi."

Giulio amewaambia wageni wa heshima akiwemo waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, na rais wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, kwamba baba yake alipigana vita vizuri na kuunga mkono mambo yasiyo sahihi akijaribu hatua ndogo baada ya nyingine kurekebisha makosa na kutafuta njia mpya. Mawaziri angalau wanane wa zamani wa Italia pia walikuwepo katika hafla ya kumuaga Napolitano.

Napolitano akumbukwa kwa kuiokoa Italia na mdororo wa kifedha

Giulio Napolitano amewaambia waombolezaji kwamba baba yake marehemu hakuweza kustahamili vitendo vya kisiasa vilivyolenga kutafuta uungwaji mkono kwa kuvutia ari na hisia za watu wa kawaida, hakuweza kuvumilia roho ya ubinafasi, wala kudunishwa kwa mijadala ya kisasa kugeuzwa kuwa kupigiana kelele, matusi, udhalilishaji na utumiaji wa lugha ya ukosoaji.

NO FLASH Italien Berlusconi Rücktritt Finanzkrise
Watu wakimshukuru Napolitano nje ya ofisi ya Silvio Berlusconi mjini Roma, Jumamosi Novemba 12, 2011, kabla Berlusocni kujiuzulu siku hiyo.Picha: dapd

Marais wa Italia mara nyingi ni viongozi wa heshima, lakini wafuatiliaji wanamsifu Napolitano kwa kuikomboa nchi  kutokana na mgogoro mkubwa wa kifedha mnamo 2011 wakati alipomshawishi waziri mkuu wakati huo, Silvio Berlusconi, ajiuzulu wakati wa mzozo wa madeni, na hivyo kuifungulia mlango serikali ya wasomi iliyoyatuliza na kuyaimarisha masoko.

Wakosoaji wanamtuhumu Napolitano kwa kuchochea mapinduzi. Berlusconi alifariki mnamo Juni, lakini mmoja wa washauri wake wa karibu, Gianni Letta, amewaambia waombolezaji kwamba anatumai viongozi hao wawili wataondoa tofauti zao na kuungana kwenye nuru watakapokutana mbinguni.

Napolitano atazikwa katika eneo dogo la makaburi lisilo la kanisa katoliki mjini Roma, mahali walipolazwa kwenye nyumba zao za milele washairi wa Uingereza, John Keats na Percy Bysshe Shelley pamoja na Antonio Gramsci, muasisi wa ukomunisti wa Ulaya.

Ingawa hakuwa mtu wa kupenda dini, Napolitano alikubaliwa kwa kiwango kikubwa miongoni mwa waumini wa kanisa Katoliki na kiongozi mkuu wa kanisa hilo Papa Francis aliishangaza familia ya Napolitano kwa kutoa heshima zake za mwisho binafsi wakati wa hafla iliyofanika bungeni wikendi iliyopita.

rtre, dpae, afpe