1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buyoya azikwa Rutovu baada ya mwili wake kurejeshwa Burundi

17 Julai 2024

Mazishi ya Pierre Buyoya rais za zamani wa Burundi yamefanyika katika kijiji chake alikozaliwa cha Rutovu mkoani Bururi, baada ya mabaki yake kurejeshwa jana kutoka chini Mali alikofia tangu mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/4iQOG
Pierre Buyoya
Aliyekuwa rais wa Burundi Pierre BuyoyaPicha: Thierry Roge/REUTERS

Ni katika kijiji chake cha kuzaliwa Rutovu mkoani Bururi kusini mwa Burundi, ambapo mabaki ya rais huyo wa zamani wa Burundi yamefanyiwa mazishi, katika hali ya faragha kubwa. Mapema mwanzoni mwa wiki hii tamko rasmi la familia yake liliwaarifu waandishi habari kuwa mazishi yatafanyika faraghani na waandishi habari hawaruhusiwi kuuhuria. Kurejeshwa kwa mwili wake hadi mazishi yake kufanyika nchini kumepokelewa kwa maoni tafautio na baadhi ya raia. 

Kaze Claude ni raia wa Burundi, anasema wakati wa utawala wa Pierre Buyoya alikuwa bado hajazaliwa lakini anakaribisha hatua ya kurusu mwili wake kuja kuzikwa nchini na kwamba licha ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili, Buyoya ni raia wa Burundi.

Mwili wa rais wa zamani Burundi Buyoya warejeshwa nyumbani


Raia mwengine Bosco Harerimana ameelezea kusikitishwa kuona Buyoya amefariki pasina kufikishwa kizimbani kujibu tuhuma za mauwaji mbali mbali zilizokuwa zikimkabili. Wengine nao walihuzunishwa na hatua ya serikali kususia mazishi hayo, wakisema licha ya kesi iliokuwa ikimkabili, Pierre Buyoya aliiongoza Burundi na alikuwa na mchango mkubwa katika kufikiwa mapatano ya usitishwaji mapigano yalopelekea wapiganaji kushirikishwa katika taasisi za uongozi.

Rais huyo wa zamani Pierre Buyoya alifariki akiwa na miaka 71 akiwa nchini Mali aliko kuwa akihudumu kama mjumbe wa Umoja wa Afrika kwa Mali na kanda ya Sahel. Buyoya atakumbukwa kwa kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini na kupeleka raia kutoka jamii ya wahutu kushirikishwa katika taasisi za uongozi baada ya kutengwa kwa muda wa miaka mingi na tawala ziloshika hatamu tangu Burundi kupata Uhuru wake. 

Mwandishi Amida Issa DW Bujumbura