Rais Xi na Abe wapo ziarani nchini China
25 Oktoba 2018Ziara ya Abe inanuiwa kurejesha mahusiano mazuri na taifa hilo la pili kwa uchumi duniani baada ya uhusiano huo kuharibika mwaka 2012 wakati Japan ilipotaifisha maeneo yalio na utata yanayopiganiwa na China.
Mahusiano hayo yameanza pole pole kurejea kuwa ya kawaida katika miezi ya hivi karibuni wakati mataifa hayo mawili yakikabiliana na ushuru mkubwa kwenye bidhaa zao uliowekwa na rais wa Marekani Donald Trump.
Abe na rais wa China Xi Jinping wanatarajiwa kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa uhusiano wa kiuchumi kati ya taifa la pili na la tatu kwa ukubwa kiuchumi duniani watakapokutana siku ya Ijumaa.
Biashara kutoka Japan zinapania kuingia katika soko kubwa lililo na ushindani la China huku China nayo ikiwa na nia ya kuingia katika ulimwengu wa teknolojia na makampuni makubwa.
Wakati wa kutiwa saini mkataba huu unaorejesha mahusiano ya China na Japan yalioharibika baada ya vita vya pili vya dunia, Li ametoa wito kwa mataifa hayo mawili kuimarisha amani ushirikiano wa nchi nyingi na biashara huru.
Kulingana na televisheni ya taifa ya China CCTV Japan na China wanajukumu kubwa katika ukuaji wa uchumi wa bara la Asia na hata dunia. Waziri Mkuu Shinzo Abe ametaka mataifa hayo kufanya kazi pamoja kuimarisha amani ya dunia pamoja na ustawi.
Hii ni ziara ya kwanza ya Abe nchini China tangu mwaka 2011.
Kabla ya kuanza ziara hiyo Abe alisema nchi yake imekuwa ikiendeleza juhudi za kuimarisha uhusiano wake na China. Abe na Xi wanatarajiwa kutia saini mikataba kadhaa katika ziara hiyo ikiwemo ile ya uwekezaji wa pamoja wa miundo mbinu katika maeneo jirani kama Indonesia na Ufilipino.
Abe amesema pia wamepanga kuzungumzia suala la Korea ya Kaskazini na maeneo yanayogombaniwa wakinuiwa kuifanya bahari ya China Mashariki mwa Asia kuwa bahari ya amani urafiki na ushirikiano.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga