1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Halmashauri kuu ya umoja wa ulaya aacha madaraka

Manasseh Rukungu25 Oktoba 2004

Rais Romano Prodi ameagana na makao makuu ya umoja wa ulaya kwa mkutano maalum wa wandishi wa habari. Anarejea nchini mwake Italia ambapo ananuwia kuzingatia shuguli mpya za kisiasa hasa za kupingana na kiongozi wa sasa wa serikali na hasimu wake mkubwa Silvio Berlusconi.

https://p.dw.com/p/CHiB
Rais wa hadi sasa wa Halmashauri kuu ya umoja wa ulaya kwenye makao makuu mjini Brussels.
Rais wa hadi sasa wa Halmashauri kuu ya umoja wa ulaya kwenye makao makuu mjini Brussels.Picha: AP

Mnamo miezi michache iliyopita kabla ya kuhitimika muda wake wa kuwa rais wa halmashauri kuu ya umoja wa ulaya Romano Prodi alionekana baadhi ya nyakati kuwa bila ya makini. Mwanasiasa huyu mwenye kuelemea upande wa kushoto Prodi, ambaye baada ya kujiuzulu wadhifa wake kama waziri-mkuu wa Italia mwaka 1999 na kuhamia Brussels, alikuwa ameshatangaza tangu muda mrefu nia ya kuvua madaraka. Ana mpango wa kuzingatia shuguli nyingine za kisiasa kuanzia mwaka wa 2006 hususan za kumfukuza madarakani kiongozi wa sasa wa serikali na hasimu wake mkubwa Silvio Berlusconi kutoka kambi ya wakonsavativ.

Rais huyu wa hadi sasa anaagana na makamo makuu ya umoja wa ulaya Brussels kwa machungu moyoni, hasa kwa sababu ya viongozi wa nchi na serikali za umoja huu kuuvunjilia mbali mradi wake wa Lisbon. Profesa huyu wa mambo ya uchumi alikuwa anakusudia kwa mradi huo, kuustawisha umoja wa ulaya kiuchumi na kuufanyia mageuzi.

Lakini serikali za kitaifa ziliuziba mara nyingi, iwapo lilishugulikiwa swala la kupitishwa maamuzi mjini Brussels. Hasa Kansela wa Ujerumani Gerhard Schröder, alikuwa akimtazama Prodi kama ni mpigaji breki. Katika upande wake Kansela Schröder alitaka kushikiwa usukani umoja wa ulaya na mwanasiasa mwenye kipaji cha kuwaongoza maofisa zaidi ya 17 000. Lakini Romano Prodi hakujitazama binasfsi kama ni kiongozi wa utawala, bali kama ni rais wa shuguli za kisiasa, aliyejitahidi kwa kila njia kuamua ni upande gani umoja wa ulaya uelekee. Lakini harakati zake hazikufua dafu.

Kansela Schröder, ambaye alimsifu binafsi Prodi kwenye mkutano wa kilele mjini Berlin, kama mwenyekiti mwaka 1999, alifanya kosa kubwa katika chaguo lake. Hata ikiwa Romano Prodi aliiandaa Italia kwa hatua kali na kwa muda wa miaka mitatu, kuanzia 1996 hadi 1999, kabla ya kujiunga na sarafu mpya ya Euro, hakuonyesha hata chembe ari kama hiyo mjini Brussels. Tayari mwaka 2000, rais Prodi alilalamika katika hotuba yake muhimu kwamba, serikali za nchi 15 za zamani, zilikuwa goigoi na zilipitisha maamuzi nje ya halmashauri kuu. Ndio maana alijaribu mara nyingi kurejesha hatamu mikononi mwake, lakini hakuwahi kufanikiwa.

Hata hivyo, katika wakati wake pia yalipatikana mafanikio makubwa, kama vile kutanuliwa kwa umoja wa ulaya kuelekea mashariki kwa nchi mpya 10 mwezi mei mwaka huu wa 2004, na uamuzi wa kuanzishwa mazungumzo pamoja na Uturuki juu ya kushirikishwa kwake kama mwanachama katika umoja huu. Lakini wa kutolewa shukurani na Bw.Prodi kwa mafanikio hayo, ni kamishina wake mmojawapo mashuhuri, mjerumani Günter Verheugen pamoja na mchango uliotolewa na kamishina wake mwingine madhubuti wa maswala ya kilimo kutoka Austria, Franz Fischler. Fanikio lingine tena wakati wa uongozi wake, lilikuwa ni kuanzilishwa kwa sarafu mpya ya Euro.

Pia chini ya uongozi wa Romano Prodi, halmashauri kuu ya ulaya ilifanikiwa mnamo kipindi cha miaka mitano, kupendekeza miswada mbali mbali ya sheria mpya mbali mbali. Isitoshe, alifanikiwa kupinga vikali matakwa ya nchi wanachama kuhusiana na nyama zilizorogwa na kichaa cha ngómbe. Mwanasiasa huyu mwenye umri wa miaka 65, ananuwia kurejea katika ngazi ya viongozi wa nchi, ambao mara nyingi walimuacha mkono wakati uliopita.