1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Gabon Omar Bongo alazwa hospitali nchini Uhispania

22 Mei 2009

Rais Bongo ameiongoza Gabon kwa muda wa miaka arobaini na moja sasa, na kuwa kiongozi aliyekaa madarakani muda mrefu zaidi barani Afrika.

https://p.dw.com/p/HvD7
Rais wa Gabon Omar Bongo.Picha: picture-alliance/dpa

Rais Omar Bongo wa Gabon ambaye ni kiongozi aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, amelazwa katika hospitali moja nchini Uhispania.Iliripotwa hjapo jana kwamba kiongozi huyo alikuwa katika hali mbaya, akiugua maradhi ya saratani.

Akiwa ziarani nchini Bosnia waziri wa mambio ya kigeni wa Uhispania Miguel Angel Moratinos, aliwaambia waandishi wa habari kuwa rais Omari Bongo mwenye umri wa miaka sabini na tatu, alikuwa akitibiwa katika zahanati moja kaskazini mwa mji wa Barcelona.

Hata hivyo nchini Gabon afisi ya rais ilitoa taarifa iliyosema kuwa rais Omar Bongo alikuwa akipumzika kwa muda mfupi nchini uhispania huku pia akifanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Habari hizi zinakuja wiki chache baada ya mahakama nchini Ufaransa kutaka kufanyiwa uchunguzi juu ya mali ya rais Bongo nchini Ufaranasa.

Uchunguzi kama huo pia utafanyiwa mali ya rais wa Kongo Brazzaville Dennis Sassou Nguesso na rais wa Guinea ya Ikweta Teodoro Obiang` Nguema.

Shirika la kupambana na rushwa -Transparency International tawi la Ufaransa linawalaumu viongozi hao kwa kutumia fedha za umma, kunua nyumba nchi za nje na pia kwa kununua magari ya kifahari, madai ambayo viongozi hao wameyakanusha.

Ripoti iliyotolewa na serikali ya Gabon iisema kuwa, ilithibitisha kuwa rais Bongo alikuwa amelazwa katika zahanati moja nchini Uhispania lakini haikutaja chochote kuhusiana na maradhi ya saratani, baada ya madai kuwa rais Bongo alikuwa akiugua saratani ya utumbo.

Pia ripoti hiyo ilisema kuwa kiongozi huyo hajafanyiwa upasuaji wowote na kuvilaumu vyombo vya habari kwa kueneza uvumi wenye lengo la kuivuruga Gabon.

Akiwa ziarani nchini Cameroon waziri mkuu wa Ufaransa Francois Fillon alisema kuwa rais Bongo alikuwa katika hali nzuri hadi kufikia mapema hapo jana.

Mnamo tarehe sita mwezi huu rais Bongo anayeitawala Gabon kwa miaka arobaini na moja sasa, alisema kuwa angesitisha kwa muda shughuli zake ili kupumzika na pia kuombleza kifo cha mkewe aliyeaga dunia mwezi machi mwaka huu.

Mkewe Edith Lucie Bongo ambaye ni mtoto wa rais wa kongo Brazzaville Denis Sassou Ngueso, aliaga dunia nchini morrocco akiwa na umri wa miaka arobaini na tano, baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Habari kutoka afisi ya rais zilisema kuwa, rais Bongo alipatwa na mshutuko baada ya kifo cha mkewe .

Tangu rais Bongo achukue mapumziko hajaonekana hadharani hata baada ya ripoti kutoka kwa afisi ya rais kusema kuwa amekuwa akiendesha shughuli zake kama kawaida.

Rais Omar Bongo alijiunga na serikali ya Gabon mwaka 1965 na kuwa makamu wa rais mwaka 1967.Bongo alichukua hatamu za uongozi nchini Gabon mwaka huo huo kufuatia kifo cha ghafla cha rais Leon Mba.

Bongo alijenga utawala imara ambao ulinufaika zaidi baada ya kugunduliwa kwa mafuta nchini Gabon hata kama ikiwa utajiri wake ulinufaisha idadi ndogo ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 1.5.

Mwandishi :Jason Nyakundi/AFPE

Mhariri :Mohammed Abdul Rahman.