1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Rais Putin akubali mwaliko wa Kim Jong Un

14 Septemba 2023

Rais wa Urusi Vladmir Putin amekubali mwaliko wa kuizuru Korea Kaskazini uliotolewa na kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un.

https://p.dw.com/p/4WK2B
Russland | Kim Jong Un und Vladimir Putin am Kosmodrom Wostotschny
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Mikhail Metzel/Russian President Press Office/dpa/picture alliance

Shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA limeripoti Alhamisi kuwa Kim alitoa mwaliko huo kwa Putin jana jioni mwishoni mwa Jukwaa la Kiuchumi la mataifa ya Mashariki huko Vladivostok.

Kwa mujibu wa KCNA, Putin amekubali mwaliko huo kwa furaha na amethibitisha nia yake ya kuendeleza historia na utamaduni wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.

Putin: Kim kutembelea viwanda vya kijeshi na kiraia

Baada ya dhifa rasmi ya jana jioni iliyoandaliwa na Rais Putin kwenye mji wa Vostochny Cosmodrome, Kim aliondoka na kuelekea kwenye kituo kinachofuata. Hata hivyo, hakuna taarifa zaidi iliyotolewa.

Putin amesema kuwa siku ya Alhamisi, Kim anatarajiwa kuvitembelea viwanda vya ndege vya kijeshi na vya kiraia katika mji wa Komsomlsk-on-Amur na kukagua meli za kikosi cha wanamaji cha Urusi zilizoko Vladivostok.

Russland | Kim Jong Un und Vladimir Putin am Kosmodrom Wostotschny
Kim Jong Un na Vladimir Putin walikutana huko Vostochny Cosmodrome mashariki ya Urusi Picha: Yonhap/picture alliance

Korea Kusini imeelezea wasiwasi na masikitiko yake kutokana na mkutano wa kilele baina ya Putin na Kim, ikisema uliangazia zaidi katika kuimarisha ushirikiano wa kijeshi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Korea Kusini Lim Soo-Suk, amesema viongozi hao wawili waliotengwa na wenye silaha za nyuklia wamekuwa wakijipanga kuzidisha makabilianoa na Marekani, licha ya tahadhari kutolewa na jumuia ya kimataifa.

Urusi inapaswa kufahamu wazi kwamba iwapo itashirikiana kijeshi na Korea Kaskazini, hali hiyo inaweza kusababisha matokeo mabaya kwenye uhusiano kati ya Korea Kusini na Urusi,'' alisisitiza Lim.

Hofu ya Korea Kusini 

Wasiwasi wa Korea Kusini unaonyesha huenda Korea Kaskazini ikapokea silaha zenye teknolojia ya hali ya juu kutoka Urusi, zikiwemo zile zinazohusiana na satelaiti za kijeshi za kijasusi, ambazo zinaweza kuongeza kitisho kinachowekwa na mpango wa nyuklia wa Kim.

Korea Kusini imesema Korea Kaskazini na Urusi zitakabiliwa vikali iwapo zitakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Südkorea  Lim Soo-suk  Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Korea Kusini, Lim Soo-SukPicha: YONHAPNEWS AGENCY/picture alliance

Marekani imeonya kuwa mkutano huo wa Jumatano kati ya Kim na Putin, huenda ukasababisha kufikiwa kwa makubaliano ya kuipatia silaha Urusi katika vita vyake na Ukraine.

Jana Kim aliapa kuisaidia Urusi kwa kila hali katika vita vyake Ukraine, hatua iliyokosolewa vikali na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu uwezekano wa Korea Kaskazini kuipatia silaha Urusi.

Urusi kwa upande wake imesema leo kuwa Marekani ni mnafiki, kutokana na kuukosoa mkutano kati ya Putin na Kim, kwa sababu yenyewe imesababisha machafuko na kupeleka silaha kwa washirika wake kote ulimwenguni. Balozi wa Urusi nchini Marekani, Anatoly Antonov, amesema Marekani haina haki ya kuifundisha Urusi jinsi ya kuishi.

(AP, DPA, Reuters)