1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Obama akutana na Rais Castro wa Cuba

21 Machi 2016

Rais Barack Obama wa Marekani ambaye anaendelea na ziara yake ya kihistoria katika kisiwa cha Cuba-ya kwanza kufanywa na Rais wa Marekani kwa karibu miaka 90, amekutana na kiongozi wa kisiwa hicho Raul Castro

https://p.dw.com/p/1IH5k
Kuba Havana Staatsbesuch US Präsident Obama
Picha: Reuters/Stringer

Kwa rais Obama ambaye aliwasili mjini Havana jana hakuna mahala pazuri zaidi pa kuonyesha kuwa mazungumzo na kujongeleana ni bora zaidi ya kuweko nchini Cuba . Anaamini hiyo ni njia bora zaidi ya kuleta mabadiliko katika taifa hilo la kikoministi badala ya kulitenga.

Lakini kwa Wacuba swali kuuu ni ikiwa serikali yao iko tayari kudhihirisha kwamba kuanzishwa tena kwa uhusiano wa kibalozi ni zaidi ya maneno matupu.

Makampuni ya Kimarekani yenye hamu kubwa ya kupata nafasi ya kuwekeza nchini Cuba hayana muda wa kupoteza. Obama alitangaza kwamba kampuni kubwa ya mtandao ya Google imesaini mkataba wa kutanuwa huduma ya Wi-FI kuweza kupata internet kwa kasi zaidi kisiwani humo- ambacho ni maili 90 kutoka jimbo la Marekiani la Florida.

Wakati ni muwafaka

Obama alikiambia kituo cha televisheni cha ABC, wakati ni muwafaka licha ya kwamba amekiri kuwepo kwa tafauti za mitazamo na maoni juu ya suala la haki za binaadamu na uhuru. Akiongeza kwamba anataka kuona yanapatikana pia maendeleo katika masuala hayo, kabla hajamaliza kabisa kipindi chake cha uongozi .

Bila shaka Obama aliyewasili Cuba akiwa na mkewe Michelle na binti zake Sasha na Malia ameweza kuzikosha nyoyo za Wacuba na Wamarekani kuhusu haja ya kuwa na amani, muelekeo ambao ameuanzisha yeye na Catsro ingawa katika hali ya tahadhari.

Kuba Präsident Raul Castro
Rais wa Cuba Raul CastroPicha: picture alliance/AP Photo/D. Boylan

Kwa hakika Wamarekani na Wacuba wanashirikiana kwa karibu zaidi hivi sasa kuliko wakati mwengine wowote tokea mapinduzi ya Cuba 1959. Lakini ingawa Wamarekani wameanza kumiminika Cuba kwa idadi kubwa kuliko hapo zamani, bado uhusiano huo hakuleta mabadiliko ambayo wacuba wengi wanayatarajia, ikiwa ni miezi 15 baada ya Obama na Castro kuamua kurejesha uhusiano wa kawaida .

Wacuba wanauhuru zaidi chini ya uongozi wa Raul Castro

Tokea aliposhika hatamu za uongozi kutoka kwa kaka yake Fidel Castro mwaka 2008, Raul Castro ameanzisha mageuzi madogo ya kiuchumi na kijamii ambayo yanaweza kuwa na matokeo mema , ingawa Wacuba na wageni wengi wanahisi yanakwenda polepole mno. Sio tu kwamba Wacuba sasa wanaweza kuwa na viwanda vyao wenyewe, lakini hata vizuizi vinavyohusiana na mitandao ya Internet na simu za mkononi vimepunguzwa na raia hivi sasa wanahisi wana uhuru zaidi wa kuyajadili matatizo yao. Ama pamoja na hayo Castro hajachukuwa hatua yoyote kufungua mlango wa kupunguza mamlaka ya chama kimoja

Obama anaamini kwamba ziara yake itasaidia mambo kubadilika na kuwa jibu kwa Wanaokosoa ziara yake nyumbani Marekani. Akiwa nchini humo rais Obama wa aliweka shada la mauwa katika sanamu la Jose Mareti, shujaa wa uhuru wa Cuba na baada ya mazungumzo na mwenyeji wake kwenye kasri la mapinduzi mjini Havana , Obama na Castro watakuwa na mkutano na waandishi habari, kabla ya kuhudhuria hafla ya pamoja kati ya wafanyabiashara wa Marekani na Cuba na karamu ya chakula cha usiku kwa heshima yake atakayoandaliwa na mwenyeji wake. Kesho rais Obama atatoa hotuba muhimu ambayo maafisa wa Cuba wanasema itatangazwa na televisheni ya taifa. Atakapohitimisha ziara yake hiyo ataelekea nchini Argentina.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, ap
Mhariri: Yusuf, Saumu