1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Museveni awashutumu wabunge kutumia fedha za COVID 19

Lubega Emmanuel DW kampala29 Aprili 2020

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amewashutumu vikali wabunge wa nchi hiyo kuamua kujipatia pesa zilizokusudiwa kusaidia katika kupambana dhidi ya ugonjwa wa COVID-19.

https://p.dw.com/p/3bYPG
Yoweri Museveni
Picha: picture-alliance/dpa/A. Novoderezhkin

Spika wa bunge la Uganda Rebecca Kadaga, aliagiza kila mbunge apokee kiasi cha dola elfu tano kutokana na mgao wa kiasi cha dola milioni tatu.

Sakata la wabunge kujipatia kiasi cha dola milioni tatu limekuwa gumzo mitandaoni tangu ilipofichuka kwamba walikuwa wanapanga kupewa pesa hizo kinyume na hali ilivyo kwa sasa ambapo sekta binafsi imechangia pakubwa fedha na vitu mbalimbali ikiwemo chakula kuwakimbilia msaada raia katika kipindi hiki cha karantini ya COVID-19.

La kushangaza ni kwamba hata baada ya wabunge wawili kuwasilisha shauri mahakamani kupinga kutolewa kwa pesa hizo, spika wa bunge alisema kuwa tayari zilikuwa kwenye akaunti zao. Rais Museveni ametaja kitendo hicho kuwa cha aibu akiwataka wabunge waliozitumia pesa hizo kwa maslahi yao wazirudishe.

Rais Museveni ameagiza pesa hizo zirudishwe mara moja na ambaye hatarudisha atakatwa mshahara.
Rais Museveni ameagiza pesa hizo zirudishwe mara moja na ambaye hatarudisha atakatwa mshahara.Picha: Reuters/J.Akena

Wananchi wamewashtumu pia wabunge kwa kile walichokielezea kuwa tamaa badala ya kutoa sehemu ya mishahara yao minono kuchangia katika kukabiliana na janga la COVID -19 kama walivyofanya wanasiasa katika mataifa mengine.

Baadhi ya wabunge waliopinga hatua hiyo wakiwemo Muwanga Kivumbi na mbunge msanii Bobi Wine walielezea kuwa walisisitiza kuwa hawakufahamishwa vyema kuhusu vyanzo na matumizi ya pesa hizo. 

Rais Museveni ameagiza pesa hizo zirudishwe mara moja na ambaye hatarudisha atakatwa mshahara. Wakati huo huo Museveni ameshutumu vitendo vya vyombo vya usalama kuwanyanyasa na kuwatesa wanasiasa wa upinzani kwa kutoa misaada ya chakula. Ameshangaa kwa nini wale wa chama tawala hawakuchukuliwa hatua sawa na hiyo. Mbunge kwa jina Francis Zake angali yuko hali mahututi mikononi mwa polisi hata baada ya mahakama moja kuagiza aachiliwe.