1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mursi wa Misri aapishwa

Mohamed Dahman30 Juni 2012

Rais Mohammed Mursi amekula kiapo Jumamosi tarehe (30.06.2012) kuwa rais wa kwanza Misri kuchaguliwa katika uchaguzi ulio uhuru na kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi baada ya kupinduliwa kwa Hosni Mubarak mwaka jana.

https://p.dw.com/p/15Ofu
In this image made from Egyptian State Television, judges from Egypt's Supreme constitutional court applaud Mohammed Morsi, center, after he was sworn in as President in Cairo, Egypt, Saturday, June 30, 2012. Islamist Mohammed Morsi has been sworn in before Egypt's highest court as the country's first freely elected president, succeeding Hosni Mubarak who was ousted 16 months ago.(Foto:Egyptian State TV/AP/dapd)
Kairo Präsident Musri VereidigungPicha: Reuters

Wakati wa kula kiapo hicho katika Mahakama ya Kikatiba mjini Cairo amesema "Naapa kwa jina la Mwenyeenzi Mungu nitaenzi kwa dhati taratibu za Jamhuri ya Misri na kuheshimu katiba na sheria pamoja na kujali maslahi ya wananchi."

Mursi anayefuata siasa za Kiislamu, katika hotuba fupi baada ya kula kiapo, ameahidi kuongoza taifa linaloongozwa na raia, chini ya misingi ya kikatiba.

Mshindi huyo wa marudio ya uchaguzi wa rais wa Juni 16 na 17 alilazimika kula kiapo kwenye Mahakama ya Katiba baada ya utawala wa kijeshi kulivunja bunge linanaloongozwa na wanachama wa Udugu wa Kiislamu, kufuatia amri ya mahakama iliotolewa mapema mwezi huu.

Mursi alikuwa tayari amekula kiapo cha ishara hapo Ijumaa mbele ya maelfu ya wafuasi wake waliofurika katika uwanja wa al-Tahrir mjini Cairo ambao ulikuwa kitovu cha uasi uliompinduwa Mubarak hapo tarehe 11 mwezi wa Februari mwaka 2011.

Rais Mursi akihutubia maelfu ya wafuasi wake.
Rais Mursi akihutubia maelfu ya wafuasi wake.Picha: Reuters

Mursi aunga mkono Wapalesina na Wasyria

Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Cairo katika hotuba yake ya kwanza ya urais, Mursi amesema anawaunga mkono Wapalestina hadi hapo watakapopata haki zao zote na ametaka kukomeshwe umwagaji damu nchini Syria.

Mursi ambaye, alijiuzulu kutoka Chama cha Udugu wa Kiislamu baada ya kushinda uchaguzi, hivi sasa anakabiliwa na changamoto ya kukabiliana na wanajeshi ambao walisimamia kipindi cha mpito baada ya kun'golewa kwa Mubarak, na ambao wanasisitiza kuendelea kushikilia madaraka makubwa .

Alipouhutubia umma katika uwanja wa al-Tahrir, amesema hatoachana na haki zozote zile zinazomhusu rais, na amewaambia wafuasi wake kwamba wao ndio chimbuko la madaraka na uhalali na kwamba hakuna mtu yoyote au taasisi itakayokuwa juu ya takwa la wananchi.

Changamoto kuu ni wanajeshi

Jeshi limechukuwa madaraka ya bunge baada ya kulivunja na pia limeunda baraza la taifa la usalama wa ndani lenye madaraka makubwa linaloongozwa na rais, lakini likihodhiwa na majenerali.

Mkuu wa Majeshi nchini MIsri Mohammed Hussein Tantawi
Mkuu wa Majeshi nchini MIsri Mohammed Hussein TantawiPicha: AP

Kwa kukubali kuapishwa katika Mahakama ya Katiba, Mursi atakuwa kama ameutambuwa uamuzi wa mahakama hiyo kulivunja bunge baada ya mahakama kuhukumu kwamba theluthi moja wabunge wamechaguliwa kinyume na sheria. Jeshi pia litakuwa na haki ya kuteuwa baraza jipya la katiba pindipo lile liloteuliwa na bunge litavunjwa na uamuzi wa mahakama unaotarajiwa kutolewa hapo Septemba Mosi.

Chama cha Udugu wa Kiislamu kimekuwa kisisitiza kwamba ni bunge pekee linaweza kuteuwa baraza la katiba.

Repoti za vyombo vya habari zinasema Mursi alikuwa akiwasiliana na jumuiya mbali mbali nchini Misri kabla ya kumteuwa waziri mkuu na baraza la mawaziri ambalo linatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuwa la wasomi.

Katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliorepotiwa takriban katika magazeti yote hapo Ijumaa Mursi ameahdi kutozigeuza taasisi za nchi hiyo kuwa za Kiislamu wakati wa utawala wake.

Mursi tayari amekutana na mkuu wa utawala wa kijeshi nchini Misri, Amiri Jeshi Mkuu Hussein Tantawi, kadhalika ujumbe wa Waislamu wa madhehebu ya Sunni wa msikiti mkuu wa Al- Azhar na ujumbe mwengine unaowakilisha Kanisa la madhehebu ya Koptik.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Miraji Othman