1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Erdogan wa Uturuki aishutumu Marekani

Admin.WagnerD29 Julai 2016

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameishambulia Marekani kwa kauli yake kuhusu jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini Uturuki kwamba inamhifadhi mtu aliyehusika na jaribio hilo.

https://p.dw.com/p/1JYeN
Türkei Aussenminister Mevlut Cavusoglu und Präsident Erdogan
Picha: picture alliance/AP Photo/F.-A. Warsameh

Akizungumza kwa ghadhabu Ijumaa (29.07.2017) katika kituo cha kijeshi huko Golbasi nje ya mji mkuu wa Ankara ambapo mashambulizi ya anga yalisababisha watu kadhaa kuuwawa wakati wa jaribio la mapinduzi lililoshindwa hapo Julai 15 amesema badala ya kusimama upande wa nchi yake Marekani imekuwa upande wa wale waliopanga njama hiyo ya mapinduzi.

Amerudia tena kauli yake ambayo hupenda kuitumia wakati anapokasirika kwamba "yanawahusu nini" na kuishutumu nchi hiyo kwa kumpa hifadhi mtu aliyepanga njama hiyo ya mapinduzi ambaye wamekuwa wakimlisha.

Erdogan amesema "Badala ya kusema" ahsante " kwa taifa langu ambalo limezima jaribio la mapinduzi mnasimama pamoja na waliopanga njama ya mapinduzi.Alipanga njama hiyo tayari mnaye nchini mwenu. Ati wanasema wana wasi wasi na kipindi cha usoni.Waungwana hawa wana wasi na kitu gani? Kwamba kutakuwa na ongezeko la watu wanaowekwa kizuizini na wanaokamatwa ? Iwapo wana hatia watakamatwa.!"

Rais huyo wa Uturuki amemshutumu afisa wa kijeshi wa Marekani ambaye amesema kamata kamata inayoendelea nchini Uturuki na kukamatwa kwa magenerali kadhaa waandamizi kufuatia jaribio la mapinduzi kutaathiri ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na nchi hiyo.

Uhusiano wa kijeshi kuathirika

Akikaririwa na vyombo vya habari vya ndani ya nchi Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani Generali Joseph Votel hususan amedokeza kwamba Marekani imepoteza wajumbe wanaohusika katika mazungumzo ya kijeshi ambao hivi sasa wako gerezani kwa tuhuma za kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi.

Generali Joseph Votel.
Generali Joseph Votel.Picha: picture alliance/ZUMA Press/Y. Bogu

Serikali ya Uturuki imekuwa ikiitaka Marekani imrudishe Uturuki Sheikh Fetullah Gulen anayeishi uhamishoni kwa hiari katika jimbo la Pennsylvania. Serikali inamtuhumu Gulen kwa kupanga njama hiyo ya mapinduzi ilioshindwa ya Julai 15 ambapo watu 290 walipoteza maisha yao.

Mhariri : Mohamed Dahman/AP/AFP/Reuters

Mhariri :Yusuf Saumu