1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Buhari amsimamisha kazi jaji mkuu

26 Januari 2019

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amemsimamisha kazi jaji mkuu wa nchi hiyo, na kuanzisha mgogoro wa kikatiba katika nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya watu barani Afrika

https://p.dw.com/p/3CEQq
Muhammadu Buhari
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mpinzani mkuu wa Buhari katika uchaguzi huo, aliyekuwa makamu wa rais Atiku Abubakar, alimtuhumu rais kwa kitendo hicho alichokiita kuwa cha "kidikteta" na kisichokuwa halali nacho Chama cha Wanasheria nchini Nigeria kikiilaani kwa kusema kuwa ni "jaribio la mapinduzi" dhidi ya katiba.

Buhari ambaye alikuwa kiongozi wa kijeshi katika miaka ya 1980 na kuchaguliwa madarakani mwaka wa 2015, atagombea kwa muhula wa pili katika uchaguzi wa Februari 16. Kuachishwa kazi kwa Walker Nkanu Samuel Onnoghen kumekuja wakati jaji huyo mkuu alikuwa akijiandaa kuwaapisha majaji wa mahakama za kesi za uchaguzi.

Walter Samuel Nkanu Onnoghen Chief Justiz für Nigeria
Jaji Mkuu Onnoghen anatuhumiwa kwa ufisadiPicha: Ubale Musa

Onnoghen anakabiliwa na kesi ya madai ya kushindwa kutangaza mali za fedha za kigeni kama wanavyotakiwa kufanya maafisa chini ya sheria ya Nigeria. Madai hayo yaliibuka wiki mbili zilizopita. Idara ya mahakama na jaji mkuu watatekeleza jukumu muhimu ikiwa kutatokea utata katika uchaguzi.

Buhari amesema hatua hiyo ya kusitishwa kazi itaendelea hadi pale kesi dhidi yake itakapokamilika. Hii ni mara ya kwanza kwa jaji mkuu kushtakiwa nchini Nigeria,ambako ufisadi umekithiri. Onnoghen anahoji kuwa mashitaka hayo hayana msingi.

Waangalizi tayari wameonya kuwa uchaguzi huo huenda uksababisha machafuko – uchaguzi wa Buhari mwaka wa 2015 lilikuwa tukio la nadra la kukabidhi madaraka kwa njia ya amani katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta – na wanadiplomasia wamewaomba wagombea wakuu kusaini ahadi ya kudumisha amani.

Taarifa ya Buhari imesema kuwa mbali na mashitaka hayo ya Onnoghen, mashirika ya usalama yamegundua biashara nyingine inayotilishwa shaka ya mabilioni ya dola kwenye akaunti zake za benki.

Jaji Ibrahim Tanko Muhammed atachukua wadhifa wa kaimu jaji mkuu. Muhammed,  kama tu rais, anatokea upande wa kaskazini wenye Waislamu wengi, wakati Onnoghen anatokea kusini ambako kuna Wakristo wengi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP