1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila Odinga ajiondoa kuwania urais

10 Oktoba 2017

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, ametangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais katika uchaguzi mpya ulioamriwa na Mahakama ya Juu hapo tarehe 26 Oktoba akilalamikia kutokuwepo mageuzi ya tume.

https://p.dw.com/p/2lase
Kenia Opposition Führer Raila Odinga NASA Koalition
Picha: Reuters/T. Mukoya

Ilikuwa ni kesi iliyofunguliwa na Odinga kwenye Mahakama ya Juu dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 ndiyo iliyopelekea kufutwa kwa matokeo hayo na kuitishwa mwengine mpya.

Wakati huo, Odinga alihoji kwamba matokeo hayo yalidukuliwa na kuharibiwa kwa makusudi ya kumnufaisha mpinzani wake, Rais Uhuru Kenyatta, wa chama tawala cha Jubilee.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa taifa hilo la Afrika Mashariki kushuhudia matokeo ya urais yakifutwa mahakamani.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Odinga amesema "tume ya uchaguzi haina dhamira ya kweli" ya kuendesha uchaguzi ulio huru na wa haki kwa kuwa haitaki kufanya mageuzi kama ilivyoagizwa kabla ya kura hiyo.

Miongoni mwa mageuzi ambayo Odinga alitaka kwanza yafanyike kabla ya kushiriki uchaguzi mwengine yalihusu kubadilisha wasambazaji vifaa vilivyotumika kutangaza matokeo ya awali na pia kuondolewa kwa maafisa wa tume ya uchaguzi ambao walituhumiwa kushiriki kuuharibu uchaguzi wa Agosti 8.

Odinga anasema tume hiyo ya uchaguzi imedhibitiwa na chama tawala cha Rais Kenyatta.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman