1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Italia wapuuza msimamo wa serikali kuhusu wahamiaji

23 Agosti 2018

Mashambulizi ya ubaguzi wa rangi yanaendelea kuripotiwa dhidi ya watu weusi nchini Italia huku serikali mpya ikifunga bandari kwa watu waliookolewa katika Bahari ya Mediterenia.

https://p.dw.com/p/33dB4
Diciotti junge Grflüchtete dürfen von Bord
Picha: Reuters/A. Parrinello

Hata hivyo siyo Wataliano wote wanaounga mkono mawazo hayo, na baadhi hata wanajitolea kuwasaidia wahamiaji hao. Mwanamke kwa jina Barbara Clemente mwenye umri wa miaka 79, amekuwa akiishi na mhamiaji mmoja kwa jina la Moriba Mamadou mwenye umri wa miaka kumi na nane kwa muda wa miezi minne.

Barbara anasema hatua ya kumchukua Mamadou ambaye ana ndoto ya kucheza kandanda la kimataifa na kuishi naye, imekuwa njia moja ya kumsaidia mtu ambaye alihitaji msaada. Yeye ni miongoni mwa idadi inayoongezeka ya Wataliana ambao wamepuuza msimamo wa serikali yao na kuomba kupewa idhini ya kuishi na wahamiaji.

Mamadou anasema alitoroka nchi yao kwa kuwa alinyimwa haki zake na hakuweza kusoma ili kujijengea maisha yake ya baadaye. " Tulipokutana kwa mara ya kwanza ili kupata kufahamiana, aliniambia kwamba naweza kwenda shule kusoma, naweza kucheza na kufanya shughuli zangu.Mimi huwa simsikilizi Waziri wa Masuala ya Ndani wa Italia. Marafiki zangu humzungumzia lakini mimi sifanyi hivyo kwa sababu simpendi."

Msemaji wa kundi linalotoa msaada wa kibinadamu la Refugees Welcome, Sara Consolata, anasema watu wa kujitolea wanataka kuwaonesha wahamiaji hao kwamba si raia wote ambao wanakubaliana na msimamo mkali wa serikali. Amesema ni wachache tu lakini wapo, na hawakubaliani na masuala haya na wanahisi kwamba wakati umefika kwa wao kuchukua hatua.

´´Tangu siku ambayo Waziri Salvini alipoamua kutoiruhusu meli iliokuwa na wahamiaji kutia nanga katika bandari ya Italia, tumeona ongezeko katika idadi ya watu ambao wanajisajili katika mtandao wetu na kuomba kuishi na wahamiaji nyumbani kwao. Ongezeko hilo limeendelea kushuhudiwa kwa wiki kadhaa.´´

Italien Migranten auf Rettungsschiff
Wahamiaji wakisubiri kushuka kwenye meli walipowasili katika Bandari ya Catania, ItaliaPicha: Reuters/A. Parrinello

Shirika hilo lilibuniwa nchini Ujerumani mwaka 2015 na linasaidia kushughulikia maombi ya watu wanaotaka kuishi na wahamiaji, na kwa sasa lina matawi yake katika mataifa kumi na sita. Tawi la Italia, ambalo husajili ombi moja au mawili kila siku yanayowasilishwa na raia wa Italia, limeshuhudia ongezeko la asilimia themanini tangu kutolewa kwa uamuzi wa Waziri wa Masuala ya Ndani nchini Italia Matteo Salvini kukirejesha chombo cha uokoaji kilochukuwa kimewabeba wahamiaji 600 kutoka Bahari ya Mediterenia, tarehe 10 mwezi Juni mwaka huu.

Mmiliki wa mkahawa katika eneo la Adria, Kaskazini mwa Veneto, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiunga mkono chama cha waziri Salvini kinachopinga wahamiaji cha League, alianza kampeni ya kupinga ubaguzi wa rangi kwa kuchapisha stakabadhi za malipo zenye mhuri wenye maandishi, ´´No to Racism, Yes to integrated Adria´´ yenye maana tukatae ubaguzi wa rangi na tukubali Adria mchanganyiko. Mfanyabiasahra mwingine aliweka matangazo kwenye gazeti la eneo hilo yakiwa na ujumbe sawa na huo.

Ingawa umaarufu wa chama hicho umekua tangu kilipoingia madarakani kwa kushirikiana na vuguvugu la Nyota Tano kufuatia uchaguzi wa tarehe 4 mwezi Machi, karibu asilimia 72 ya Wataliano wanaunga mkono kanuni za hifadhi, huku asilimia 62 wakieleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ubaguzi wa rangi. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Utafiti la Ipsos MORI:

Hata hivyo, utafiti huo umeonesha kwamba ni asilimia 18 pekee wanaochukulia athari za uhamia nchini humo kwa mtizamo mzuri. Lakini licha ya ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutoa misaada, Waziri wa Masuala ya Ndani wa Italia Matteo Salvini, ambaye kauli yake mbiu, Wataliano kwanza, inafananishwa na ile ya Rais wa Marekani Donald Trump ya Marekani Kwanza, ametangaza kuwa serikali itaweka kikomo kwenye msaada wa kiserikali wanaopata wahamiaji waliopewa hadhi ya ukimbizi. Vile vile ameapa kwamba atapunguza msaada kwa wanaotafuta hifadhi nchini humo.

Msimamizi wa huduma za wahamiaji anayeishi mjini Rome, Paolo Morozzo della Rocca, amesema ni kinyume kuwaweka wahamiaji katika njia panda bila kuwasaidia kujenga maisha yao.

Mwanandishi: Sophia Chinyezi/APE

Mhariri: Iddi Ssessanga