1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Propaganda za siasa kali kuathiri uchaguzi wa bunge la Ulaya

Sylvia Mwehozi
22 Mei 2019

Mamilioni ya wapiga kura wa Ulaya wanakabiliwa na kitisho cha propaganda za vyama vya siasa kali katika mtandao wa Facebook kuelekea uchaguzi wa bunge la Ulaya utakaofanyika wiki hii. 

https://p.dw.com/p/3IrxG
Symbolbild Facebook Fake News
Picha: picture-alliance/L. Huter

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali ya Avaaz yenye makao yake makuu Marekani, ni kwamba habari za uongo, na video fupi zilizowasilishwa kama ushahidi wa vitendo vya wahamiaji ni mojawapo ya mbinu zinazotumiwa na kurasa za Facebook za vyama vya siasa kali. Taarifa hizo za uongo zilitazamwa mara milioni 533 katika kipindi cha miezi mitatu pekee au mara milioni sita kwa siku kwa mujibu wa asasi ya Avaaz.

Wakati wapiga kura barani Ulaya wakijiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa bunge wiki hii, Umoja wa Ulaya "umezama katika habari za uongo", alisema mkurugenzi wa kampeni wa asasi hiyo Christoph Schott. "Ukubwa na upana wa hiyo mitandao unazifanya kuwa silaha zinazoangamiza demokrasia na hivi sasa zimeelekezwa kikamilifu Ulaya", alisema mkurugenzi huyo.

Asasi hiyo iligundua kurasa karibu 500 za propaganda na makundi mbalimbali mitandaoni wakati ilipofanya utafiti wake nchini Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Uhispania, Poland na Italia. Kampuni ya Facebook tayari imezifuta kurasa 77 kati ya hizo, ambazo zilikuwa na jumla ya wafuasi milioni 5.9.

Brüssel EU-Parlament | Mark Zuckerberg, Facebook-CEO
Mkurugenzi wa Facebook Mark ZuckerbergPicha: picture-alliance/AA/European Parliament

Vidio na hotuba za chuki 

Kama mojawapo ya mifano ya propaganda za siasa kali iliyogunduliwa na asasi ya Avaaz ni ukurasa mmoja wa Italia ambao unaunga mkono chama cha Matteo Salvini cha League Party. Ukurasa huo ulichapisha vidio inayoonyesha wahamiaji wakiharibu gari ya polisi. Vidio hiyo kiuhalisia ni kipande cha filamu, ambacho kilikwisha ripotiwa lakini bado kipande hicho kinasambazwa. Kipande kama hicho cha vidio pia kilitumiwa nchini Poland kueneza habari ya uongo kuhusu dereva taxi mwamiaji anayedaiwa kumbaka mwanamke.

Soma zaidi...

Mbinu nyingine inayotumiwa na kurasa za vyama vya siasa kali nchini Uhispania na kwingineko ni kuanzisha makundi yanayopewa majina ya kuwarubuni watumiaji na kisha kuwawakea maudhui ya siasa za vyama hivyo. Mbali ya kuzifuta kurasa 77, Facebook pia imeziondoa kurasa 230 za watu binafsi tangu ilipotaarifiwa na Avaaz. Inaeleza zaidi kuwa "Facebook lazima ihakikishe kila mmoja aliyefikiwa na taarifa hizo za uongo anapokea taarifa ya masahihisho ili kuondoa sumu inayoenea".

Ripoti hiyo inasema kwa ujumla raia wengi wa Ulaya wamekumbana na taarifa za uongo, udanganyifu na hata hotuba za chuki na kama facebook haitachukua hatua madhubuti basi habari hizo za uongo zitaendelea kujitokeza katika kila uchaguzi.