1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo asema Hezbollah ni kitisho Mashariki ya Kati

21 Machi 2019

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amelielezea kundi la Hezbollah la Lebanon kama kitisho kwa ajili ya utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati. Kauli hiyo ameitoa wakati akiwa anajiandaa kuizuru Lebanon.

https://p.dw.com/p/3FRPK
Mike Pompeo
Picha: Reuters/A. Harnik

Pompeo ameyasema hayo siku ya Jumatano akiwa nchini Israel katika ziara yake ya Mashariki ya Kati yenye lengo la kukazia msimamo wa utawala wa Marekani dhidi ya Iran ambayo inaliunga mkono kundi la Hezbollah la Lebanon, kundi la Hamas la Palestina na waasi wa Houthi wa Yemen. Katika mkutano wake na Rais wa Israel, Reuven Rivlin mjini Jerusalem, Pompeo ameyaorodhesha makundi hayo kama taasisi ambazo zinasababisha hatari katika utulivu wa Mashariki ya Kati na Israel.

''Umeizungumzia Hamas, Hezbollah na Houthi. Wote hao wanasababisha hatari katika Mashariki ya Kati. Wamedhamiria kuiondoa Israel katika uso wa dunia na tuna wajibu wa kuzuia hilo lisitokee. Mnapaswa kufahamu kwamba Marekani imejiandaa kufanya hivyo, '' alibainisha Pompeo.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Hezbollah 

Kwa upande wake Israel imefanya mashambulizi ya mara kwa mara ya anga dhidi ya kundi la Hezbollah nchini Syria, ambako kundi hilo la Waislamu wa madhehebu ya Kishia pamoja na majeshi ya Urusi yanamsaidia Rais wa Syria, Bashar al-Assad kupambana na kundi la waasi na makundi ya wapiganaji yenye Waislamu wengi wa madhehebu ya Sunni.

Aidha, Rivlin amesema Waziri Mkuu wa Lebanon, Saad al-Hariri hawezi kumueleza mtu yeyote kwamba nchi hiyo imejitenga na kundi la Hezbollah. Rivlin amesema iwapo kitu chochote kitatokea kutoka Lebanon kuelekea Israel, basi Lebanon itawajibika. Kundi la Hezbollah lina wawakilishi katika baraza la mawaziri pamoja na bunge la Lebanon.

Hassan Nasrallah
Kiongozi wa Hezbollah nchini Lebanon, Hassan NasrallahPicha: picture alliance/AP/H. Malla

Hayo yanajiri wakati ambapo Pompeo kesho Ijumaa anatarajiwa kukutana na Rais wa Lebanon, Michel Aoun na spika wa bunge la nchi hiyo, pamoja na waziri wa mambo ya nje. Maafisa hao wote watatu wa ngazi ya juu ni washirika wa karibu wa Hezbollah. Pia mwandiplomasia huyo wa Marekani atakutana na Waziri Mkuu Hariri, mshirika wa karibu wa mataifa ya Magharibi na ambaye amekuwa akisita kukabiliana na Hezbollah.

Pompeo anatarajia kuitumia ziara yake hiyo ya kwanza nchini Lebanon kuongeza shinikizo dhidi ya Iran pamoja na mshirika wake, kundi la Hezbollah. Amesema watatumia muda mwingi kuzungumza na serikali ya Lebanon kuona jinsi wanavyoweza kuisaidia kujitenga na kitisho kinachowekwa kwao na Iran pamoja na Hezbollah.

Katika muongo mmoja uliopita, Marekani imekuwa ikiliunga mkono kwa kiasi kikubwa jeshi la taifa la Lebanon kwa kuwapatia silaha na msaada wa zaidi ya Dola bilioni 1.5. Lakini Hezbollah, kundi pekee ambalo halijasalimisha silaha baada ya vita vya wenyewe kwa kwenyewe kuanzia mwaka 1975 hadi 1990, linapongezwa kwa kumaliza uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon mwaka 2000 na limesema ndilo kundi lenye nguvu na uwezo wa kuzuia uvamizi mwingine wa Israel.