1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi wachunguzwa kuhusu miili iliyotupwa Kenya

Josephat Charo
13 Julai 2024

Mamlaka huru inayosimamia jeshi la polisi nchini Kenya IPOA imesema inachunguza polisi waliohusika kwa njia yoyote kufuatia ugunduzi wa miili iliyokatwakatwa na kutupwa kwenye shimo la jalala mjini Nairobi.

https://p.dw.com/p/4iFg3
Maafisa wa polisi na wa usalama wakishika doria kulilinda jengo la bunge la Kenya wakati waandamanaji walipoingia Juni 25, 2024.
Maafisa wa polisi na wa usalama wakishika doria kulilinda jengo la bunge la Kenya wakati waandamanaji walipoingia Juni 25, 2024.Picha: LUIS TATO/AFP

Awali polisi walisema miili kadhaa iliyokatwakatwa ya wanawake sita iliyofungwa kwenye mifuko ya plastiki ilipatikana siku ya Ijumaa ikiwa imetupwa kwenye jalala la taka katika timbo isiyotumika huko Mukuru, kusini mwa mji mkuu, Nairobi.

Mamlaka ya IPOA ilisema katika taarifa baadaye kwamba mabaki ya watu wapatao tisa ilikuwa imegunduliwa, saba ya wanawake, na kuitisha uchunguzi wa haraka ufanyike kuitambua.

"Miili iliyofungwa kwenye mifuko na kamba za nailoni, ilikuwa na alama za wazi za mateso ya kukatwakatwa," ilisema mamlaka hiyo, ikidokeza kwamba jalala hilo lilikuwa chini ya mita 100 kutoka kituo cha polisi.

Polisi ya Kenya wanakabiliwa na ukosoaji na shinikizo baada ya watu kadhaa kuuliwa wakati wa maandamano ya mwezi uliopita, huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiwatuhumu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Kamanda wa jeshi la polisi Japhet Koome, aliyelengwa sana katika ghadhabu ya umma kuhusiana na vifo hivyo, amejiuzulu chini ya miaka miwili tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, afisi ya rais ilitangaza Ijumaa.

Ni kiongozi wa hivi karibuni wa cheo cha juu kuachia ngazi huku rais William Ruto akijitahidi kudhibiti mgogoro mbaya kabisa wa utawala wake, uliosababishwa na mapendekezo ya kuongeza kodi uliokosolewa sana.

Kamanda Mkuu wa jeshi la polisi Kenya aliyejiuzulu, Japhet Koome
Kamanda Mkuu wa jeshi la polisi Kenya aliyejiuzulu, Japhet KoomePicha: AP Photo/picture alliance

Umati wa watu waliokusanyika Ijumaa katika eneo kulikopatikana miili walikuwa wakipiga kelele wakisema "Ruto lazima aende", kauli mbiu ya wimbi la maandamano yaliyoongozwa na vijana Wakenya wenye umri mdogo wa vuguvugu la Gen-Z.

Polisi ya Kenya wanaogopwa na hukabiliwa na madai ya mara kwa mara ya mauaji kinyume cha sheria lakini ni nadra kushtakiwa na kuhukumiwa.

Picha za kutisha

Picha kwenye televisheni nchini humo ziliwaonyesha watu wakitumia kamba kuopoa magunia yaliyokuwa na mabaki ya miili ya binadamu kutoka kwenye maji yaliyojaa taka katika jalala la kwenye timbo huko Mukuru.

"Huku uchunguzi wa polisi ukiendelea, IPOA kwa uangalifu inafanya uchunguzi wa awali kubaini kama kulikuwa na uhusikaji wowote wa polisi katika vifo hivyo, au kushindwa kuchukua hatua kuvizuia," mamlaka hiyo ilisema.

Soma pia: Koome awashutumu wanasiasa kwa kukodisha maiti kulichafulia sifa jeshi la polisi

Kurugenzi ya uchunguzi wa makosa ya jinai imesema uchunguzi unapendekeza wahanga wote waliuwawa kutumia mfumo sawa, bila kutoa maelezo.

Afisi ya muendesha mashitaka ya umma pia iliangazia eneo ilipopatikana miili hiyo kuwa karibu sana na kituo cha polisi na kusema ina wasiwasi mkubwa kuhusu ugunduzi huo unaoashiria "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu".

Imeelekeza polisi iwasilishe matokeo ya uchunguzi wao katika kipindi cha siku 21, na pia kuzihimiza wakala za dola ikiwemo mamlaka huru ya IPOA kufanya uchunguzi kuhusu ripoti za watu kupotezwa kwa kutumia nguvu na vifo vinavyodaiwa kufanywa na polisi.

Tume ya haki za binadamu ya Kenya, asasi isiyo ya kiserikali, ilisema ilikuwa pia inahimiza uchunguzi wa kina ufanyike kubaini chanzo cha vifo hivyo na kuwatambua waliohusika.

(afp)