1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paraguay yafungua ubalozi wake Jerusalem

21 Mei 2018

Paraguay imefungua ubalozi wake nchini Israel katika mji wa Jerusalem Jumatatu na kuifanya kuwa nchi ya tatu kuhamisha ubalozi wake Tel Aviv katika hatua hiyo ya kisiasa inayoweza kuibua hisia kali.

https://p.dw.com/p/2y4PC
Israel vor Eröffnung der paraguayische Botschaft in Jerusalem
Picha: Reuters/S. Scheiner

Rais wa Paraguay, Horacio Cartes, na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walihudhuria sherehe hiyo ya ufunguzi wa ubalozi huo, huku viongozi wa Palestina wakiyatolea wito mataifa ulimwenguni kuiwekea vikwazo Paraguay.

Marekani iliuhamishia ubalozi wake mjini Jerusalem wiki moja iliyopita na kusababisha hasira kutoka kwa Wapalestina. Ilifuatiwa na Guatemala iliyofanya hivyo Jumatano. Na sasa Paraguay imefuata mkumbo katika tukio ambalo Rais Horacio amelitaja kuwa ni la kihistoria na linaloongezea nguvu uhusiano wa nchi hizo mbili.

"Hafla hii ina maana kubwa sana kwa sababu inawakilisha urafiki wa dhati kabisa na uungaji mkono wa Paraguay kwa Israel," alisema Rais Horacio. "Upendo nilionao kwa taifa hili muhimu na jasiri umejengwa kwa misingi ya maadili na misimamo ambayo inalingana na yetu," aliongeza Rais huyo wa Paraguay.

Hatua ya Paraguay ni jambo zuri kwa israel na Paraguay

Katika taarifa yake, Hanan Ashrawi ambaye ni afisa mkuu katika utawala wa Palestina ulioko Ukingo wa Magharibi amesema hatua hiyo ya Paraguay ni ya kuchochea na isiyo na maana. Ameandika na hapa namnukuu "Paraguay imepanga na Israel na Marekani pamoja na Guatemala kuitilia mkazo hatua ya kuikalia ardhi hii na kuufunga mjadala wa umiliki wa Jerusalem Mashariki," mwisho wa kunukuu.

Israel vor Eröffnung der paraguayische Botschaft in Jerusalem
Rais wa Paraguay Horacio Cartes (kushoto) na Rais wa Israel (Reuven Rivlin (kulia)Picha: Reuters/R. Zvulun

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameitaja hatua ya Paraguay kama siku nzuri kwa Israel na Paraguay.

"Nataka kuanza na kumsalimia rafiki mkubwa wa Israel na rafiki yangu mkubwa Rais Horacio Cartes Jara wa Paraguay," alisema Netanyahu. "Ulikuja kuniona nilipokuwa Buenos Aires, sisahau hilo na sasa unakuja hapa kuufungua ubalozi - ni siku njema kwa Israel, siku njema kwa Paraguay na siku njema kwa urafiki wetu," alisema Waziri mkuu huyo wa Israel.

Israel iliichukua nusu ya Jerusalem Mashariki katika vita vya mwaka 1967 vya Waarabu na Waisraeli na kulivamia eneo hilo katika hatua ambayo haikutambuliwa kimataifa. Palestina inataka Jerusalem Mashariki iwe mji wake mkuu na eneo hilo ndilo kikwazo kikuu katika kupatikana kwa amani kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Huenda Abbas akatolewa hospitali Jumanne

Wakati huo huo, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas bado amelazwa katika hospitali moja Ukingo wa Magharibi huku maafisa wakisema hali yake inaendelea kuwa nzuri. Abbas, mwenye umri wa miaka 83, alilazwa jana baada ya kiwango chake cha joto mwilini kupanda kufuatia upasuaji wa sikio aliofanyiwa Jumamosi. Kuzorota kwa hali ya kiongozi huyo mkongwe kunahofiwa kuwa kunaweza kuidhoofisha Palestina katika mapambano yake na Israel.

Palästinenser Präsident Mahmoud Abbas
Rais wa Palestina Mahmoud AbbasPicha: Reuters/M. Torokman

Lakini mbunge aliye karibu na rais huyo amesema huenda akatolewa hospitali Jumanne, ingawa hakuzungumzia ugonjwa alionao. Abbas ana historia ndefu ya matatizo ya kiafya. Aliwahi kukumbwa na matatizo ya moyo na saratani ya tezi dume. Mwaka jana alifanyiwa upasuaji wa moyo wa dharura baada ya kukabiliwa na uchovu mwingi na maumivu ya kifua.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/DPAE/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef