1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa akutana na wahamiaji kisiwani Lesbos

5 Desemba 2021

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis leo amekitembelea kwa mara nyingine kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki eneo ambalo lilikuwa kitovu cha wimbi la wahamiaji miaka 6 iliyopita

https://p.dw.com/p/43rYO
Griechenland | Besuch Papst Franziskus
Picha: AFP

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis leo amekitembelea kwa mara nyingine kisiwa cha Lesbos nchini Ugiriki eneo ambalo lilikuwa kitovu cha wimbi la wahamiaji miaka 6 iliyopita na kuitaja tabia ya kuwapuuza wahamiaji kuwa ni "kwenda mrama kwa ustaarabu" duniani.

Papa Francis ambaye alitumia muda wa saa mbili kukizuru kisiwa hicho chenye kiasi waomba hifadhi 2,200 ameonya kuwa bahari ya Mediterrania inageuka kuwa eneo la makaburi lisilo na mawe na ulimwengu haujabadilika vya kutosha linapokuja suala la uhamiaji.

Akizungumza katika kambi ya wakimbizi ya Mavrovouni kisiwani hapo, kiongozi huyo wa kanisa Katoliki alisema "Barani Ulaya kuna wale wanaosisitiza katika kulishughulikia tatizo hilo kuwa suala lisilowahusu."

Papa Francis amesema sababu za msingi zinapaswa kushughulikiwa – siko watu maskini wanaolipigia gharama za mzozo huo na hata kutumika kwa propaganda za kisiasa.

Griechenland - Papst auf Lesbos
Papa Francis akiwasili katika kambi ya wakimbizi ya Mavrovouni kwenye kisiwa cha LesbosPicha: Guglielmo Mangiapane/REUTERS

Ziara yake kwenye kisiwa hicho ni sehemu ya ziara yake ya siku tano nchini Cyprus na Ugiriki na imefanyika siku moja tangu alipotoa mataashi makali ya kukemea siasa za kizalendo alizosema zinatishia ustawi na demokrasia barani Ulaya

Soma zaidi: Papa Francis : Siasa za kizalendo ni kitisho kwa demokrasia

Umoja wa Ulaya umenasa katika mzozo na Belarus kuhusu mmiminiko wa wahamiaji wanaosafiri kupitia taifa hilo lililokuwa sehemu ya muungano wa Kisovieti wakitaka kuingia Poland, Lithuania na Latvia katika miezi ya karibuni.

"Ziara yake ni baraka," amesema Rosette Leo, muomba hifadhi wa Kikongo aliyekuwepo eneo hilo. Hata hivyo, Menal Albilal, mama wa Kisyria mwenye mtoto wa umri wa miezi miwili ambaye ombi lake la hifadhi lilikataliwa miaka miwili iliyopita kisiwani hapo, amesema wakimbizi "wanataka vitendo na sio maneno matupu, wanataka msaada."

Nchini Cyprus, ambako Papa Francis alizuru wiki hii kabla ya kwenda Ugiriki, maafisa wamesema wahamiaji 50 watahamishiwa Italia.

Alipokitembelea kisiwa cha Lesbos mwaka 2016, Papa Francis aliwachukua wahamiaji 12 kutoka Syria na kuondoka nao kwa kutumia ndege rasmi inayomsafirisha.

Kwa kutumia fedha za Umoja wa Ulaya, Ugiriki unajenga msururu wa vituo vya muda kwenye visiwa vya Ugiriki kwa kutumia nyaya za miba, kamera za siri, masjhine za uchunguzi wa X-Ray na malango ya smaku ambayo yanafungwa usiku. Kambi za aina hii zimefunguliwa kwenye visiwa vya Samos, Leros na Kos huku Lesbos na Chios vikifuata mwaka ujao.

Mara baada ya waomba hifadhi wanatambuliwa kama wakimbizi, hawahitajiki tena kubakia kambini humo.

AFP