"Obama ni kiongozi mujarabu"
7 Novemba 2012Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema Ujerumani na Marekani zimekuwa zinashirikiana vizuri katika sera za mambo ya nje. Waziri Westerwelle amesema hayo baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Rais nchini Marekani ambapo Rais Obama amechaguliwa kwa kipindi kingine.
Waziri huyo wa Ujerumani alitoa kauli hiyo mjini New York ambako anafanya mazungumzo kwenye Umoja wa Mataifa. Westerwelle amesema Ujerumani na Marekani zina maslahi mengi ya pamoja. na kwamba nchi hizo zina mambo mengi ya kuyafanya kwa pamoja katika siku za usoni.
Waziri huyo wa Ujerumani amesema baada ya uchaguzi kufanyika nchini Urusia na baada ya kumalizika kipindi cha tashwishi nchini Marekani, sasa inazipasa Ujerumani na Marekani kutumia fursa iliyopo ili kuendeleza juhudi za kupunguza silaha.
Waziri huyo wa Ujerumani anatumai kwamba siasa ya kukwamishana ndani ya Marekani haitaendelezwa.Ameeleza kuwa wajumbe wengi wa jumuiya ya Tea Party hawakuchaguliwa tena, na kwa hivyo, amesema sasa inawezekana kushirikiana.
Juu ya mgogoro wa madeni Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ametoa mwito kwa Marekani na Ulaya wa kushirikiana katika kuukabili mgogoro huo.Amesema pande mbili hizo zinapaswa kukomesha sera ya madeni.
Marekani bado haijaanza kutekeleza sera ya kurebisha bajeti sambamba na kuendeleza ustawi.Njia hiyo ya kuleta ustawi imeshaanza kutekelezwa katika nchi za Ulaya.Na kwa ajili hiyo Waziri Westerwelle ametoa mwito wa kuendeleza zaidi biashara huru baina ya Marekani na Ulaya.
Ametaka mazungumzo juu ya suala hilo yaanzishwe haraka.
Katika salamu za pongezi kwa Obama Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametilia maanani uhusiano mzuri uliopo baina ya Ujerumani na Marekani.Kansela Merkel amesema katika pongezi zake kwamba Ujerumani na Marekani zimeshirikiana kwa undani na kirafiki katika miaka iliyopita.
Amesema anathamini sana mazungumzo aliyoyafanya baina yake na viongozi wa Marekani na anafurahia kuyaendeleza mazungumzo hayo. Kansela wa Ujerumani amemwalika Rais Obama kufanya ziara nchini Ujerumani.
Kiongozi wa wabunge wa chama kikuu cha upinzani Frank - Walter Steinmeier amefurahishwa juu ya kuchaguliwa tena kwa Rais Obama. Bwana Steinmeier amesema Obama ni kiongozi mujarabu kwa Marekani.
Mwandishi: Scholz,Kay-Alexander
Tafsiri: Mtullya Abdu.
Mhariri: Saumu Mwasimba