Obama aonyesha ufasaha, lakini mageuzi NSA yatafuata?
18 Januari 2014Tofauti hiyo ilichora mstari katika hotuba ya Obama iliyosubiriwa kwa hamu juu ya kudhibiti shughuli za shirika la usalama wa taifa la Marekani NSA siku ya Ijumaa, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa inaonyesha taswira ya urais wake katika mfano mdogo. Mwisho wake, licha ya hatua ambazo Obama amechukuwa au kuahidi kuchukuwa--ilikuwa bado haijawa bayana iwapo mageuzi hayo -- yakiwemo kupunguza lakini siyo kukomesha kabisa ukusanyaji wa taarifa za simu --yalikuwa ya kiishara tu au muhimu.
"Ingawa tumetiwa moyo na hatua kadhaa chanya ambazo rais amezibainisha leo, maswali mengi na mageuzi muhimu yaliachwa bila kutolewa majibu," alisema Sascha Meinrath, mkurugenzi wa taasisi huria ya teknolojia ya mfuko wa Marekani Mpya. "Masuala kadhaa yanayozua ubishani yamesukumwa kwa bunge au kwa maafisa wengine wa serikali."
Arefusha mjadala
Kwa kuwatolea wito wabunge na wadau wengine muhimu kama NSA na wizara ya sheria kujiunga na mjadala, Obama alihakikisha kuwa malumbano juu ya mageuzi katika shirika la usalama wa taifa NSA yaliyoligawa taifa hilo, yanaendelea kwa muda mrefu. Bado haiko wazi Obama yuko tayari kutunisa misuli kiasi gani ili kuyafanya mageuzi hayo kuwa sheria.
Hotuba ya Ijumaa, kama zilivyo nyingi za huko nyuma, ilionyesha upande wa kisiasa wa Obama, kama mtu mwerevu, muunganishi, asiotishika, licha ya mapambano makali na wapinzani wake kutoka chama cha Republicans, na madai kwamba yeye ndiye kiongozi wa Marekani aliewagawa zaidi raia katika kipindi cha miongo kadhaa.
Obama alijionyesha kama myakinifu anaeiongoza nchi yake kupita katika eneo lililojaa miiba, ili kufungamanisha vita dhidi ya ugaidi na misingi ya kuanzishwa kwa taifa la Marekani. Alifuata kanuni inayofahamika yenye utaratibu, akizungumza kwa sauti ya ueledi na kuchomekea maneno ya kisheria na kupuuza hoja za wapinzani.
Atumia hadithi za kihistoria kujenga hoja
Obama ambaye alijijengea umaarufu kutokana na kipaji chake cha kuzungumza, mara nyingi hutumia hadithi za historia katika hotuba zake. Siku ya Ijumaa, kabla ya kujadili kazi ya majajusi wa Marekani wanaotoa taarifa za mapema kuonya dhidi ya mashambulizi ya kigaidi, alimnukuu Paul Revere, ambaye alionya juu ya kusonga mbele kwa wanajeshi wa adui Uingereza wakati wa vita vya uhuru.
Baada ya kutengeneza mandhari, alirudi katika suala la wakati huo: Ni nini Marekani inapaswa kufanya kufuatia ufichuzi mkubwa uliyofanywa na mfanyakazi wa zamani wa NSA Edward Snowden, kuhusu udukuzi wa nchi hiyo? Alichora taswira ya siku zilizofuatia mashambulizi ya Septemba 11, 2001 wakati majajusi wa Marekani walipowekewa mbinyo kuzuwia shambulizi jengine.
"Hata hivyo, katika kukurupuka kwetu kushughulikia vitisho halisi, hatari ya serikali kuvuka mipaka -- yaani uwezekano kwamba tunapoteza baadhi ya haki zetu za msingi katika kuhakikisha usalama --zilizidi kujidhihirisha," alisema. Jibu lake kwa tatizo lilikuwa Obama wa kiwango cha juu.
Akiwa amebanwa katikati ya mashirika ya ujasusi kwa upande mmoja na makundi ya haki za kiraia kwa upande mwingine, alipendekeza njia ya kati. "Wale wanaosumbuliwa na programu zetu za sasa hawataki kurudiwa kwa matukio ya Septemba 11, na wale wanaotetea programu hizi siyo kwamba wanapuuza haki za kiraia," alisema.
Kupunguza na siyo kukomesha udukuzi
Obama analenga kupunguza baadhi ya mamlaka lililonayo shirika la NSA, lakini hatua hiyo haitakomesha kabisa udukuzi wa mawasiliano ya simu. Katika namna sawa na hiyo, Obama alitangaza kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Afghanistan mwaka 2009, lakini wakati huo huo alibainisha tarehe mwaka 2011, ya vikosi kurudi nyumbani.
Hata mpango wake anaojivunia wa afya uliwakilisha tahfifu kati ya matumaini ya wafuasi wa kiliberali, na aina ya mpango uliyoweza kuwa--ili--kupita tu. Hisia zilizotolewa juu ya hotuba ya Obama zilionyesha wasiwasi juu ya umbali gani mageuzi hayo yanaweza kufika.
"Wakati mageuzi hayo ya kiutaratibu juu ya ukusanyaji wa data yanakaribishwa, hayakidhi matarajio ya kukomesha programu hiyo kama alivyodai rais," alisema Brett Solomon, mkurugenzi mtendaji wa shirika linalotetea haki za kidigitali, na kuongeza kuwa, "mageuzi ya kweli yanahitajika, na yanahitajika sasa hivi."
Acheza na saikolojia
Obama alitumia hotuba yake kujibu hoja pinzani dhidi ya mawazo yake, na baadae kuzipuuza. "Hatuwezi kuyanyan'ganya nyenzo mashirika yetu ya ujasusi," alisema Obama kuwaambia wale wanaotaka kukomeshwa kabisaa kwa ukusanyaji mkubwa wa data. Kwa wale wanaotaka mageuzi, alisema: "Mfumo wetu wa serikali umejengwa kwa msingi kuwa uhuru wetu hauwezi kutegemea nia njema ya wale walioko madarakani, bali unategemea sheria kuwadhibiti wale walioko madarakani."
Katika mbinu nyingine iliyozoeleka, Obama pia alizilenga pande tofauti. Aliwasifu majasusi wa Marekani, uaminifu wa makundi ya haki za kiraia, aliwashambulia washirika wa Marekani kwa kulalamikia udukuzi wa Marekani na pia alitoa ishara kwa "bwana Snowden" kwamba asitarajie msamaha.
Na alizipiga vijembe Urusi na China, akisema hazingeweza kuruhusu mjadala kuhusu uchunguzi, kabla ya kumalizia kwa wito wa kuwepo malengo na maadili sawa ya kitaifa. "Pamoja tutafute njia ya kusonga mbele ambayo inahakikisha usalama wa maisha yetu kama taifa, wakati tukilinda haki zinazotupa sababu ya kulipigania taifa letu."
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Bruce Amani