1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nigeria: Wafanyakazi na serikali wakubaliana kufuta mgomo

28 Septemba 2020

Vyama vya wafanyakazi Nigeria vimekubaliana na serikali kuufuta mgomo uliopangwa wa kupinga ongezeko la bei ya mafuta ya petroli na gharama ya umeme.

https://p.dw.com/p/3j6OG
Nigeria Öl Politik Protest
Picha: Getty Images/AFP/P. Utomi Ekpei

Pande hizo mbili zimeafikiana saa kadhaa kabla ya mgomo huo uliotarajiwa kuzifunga biashara nchini humo. 

Tangazo la kufutwa kwa mgomo huo limetolewa Jumatatu na waziri wa kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi.

Baraza la kazi nchini Nigeria NLC ambalo linawawakilisha mamilioni ya waajiriwa wa sekta mbali mbali katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Afrika,ikiwemo baadhi ya sekta ya mafuta wiki iliyopita lilitangaza kuanzisha mgomo wa nchi nzima.

Katika mwezi huu wa Septemba Nigeria ilipunguza kwa kiwango kikubwa gharama ya ruzuku ili kuruhusu bei ya mafuta ya Petroli kuamuliwa na soko na kuongeza kiwango cha bei ya umeme.

Rais Muhammadu Buhari alisema Nigeria haiwezi tena kugharimia ruzuku lakini vyama vya wafanyakazi vilisema nchi hiyo inahitaji kuibatilisha  hatua ya kuongeza bei ya mafuta ili kuepuka mgomo.